Mkurugenzi wa Spicenet Tanzania, Viney Choundary akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu mashindano
ya wazi ya kimataifa yajulikanayo kama ‘Spicenet Tanzania Open Chess
Championship 2013’ yanayotarajiwa kutimua vumbi juni 14-16 katika ukumbi wa Meru uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam. Kulia ni Emmanuel Mwaisumbe na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha mchezo wa Chess, Joe Anea.
Emmanuel Mwaisumbe akifafanua jambo.
Na Elizabeth John
CHAMA cha Mchezo wa Chess nchini, kimeandaa
mashindano ya wazi ya kimataifa yajulikanayo kama ‘Spicenet Tanzania Open Chess
Championship 2013’ ambayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 14 hadi 16
katika ukumbi wa Meru uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower mtaa wa Ohio
jijini Dar es Salaam
Katika kunogesha mashindano hayo ambayo yataweka
rekodi Afrika Mashariki, yatashirikishwa na bingwa ambaye alikua ni mchezaji
namba tatu duniani mwaka 1990, Nigel Short.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chess, Joe Anea alisema mashindano hayo
yatahusisha wachezaji kutoka Tanzania, Zambia, Uganda na Kenya na kwamba
yanatarajiwa kuhudhulia na jumla ya wachezaji 80, huku wachezaji 50 wakitoka
Tanzania na 30 kutoka nchi za jirani.
Alisema kuwa mshindi wa kwanza atajinyakulia sh.
1,000,000, sh.500,000 kwa mshindi wa pili, sh. 300,000 kwa mshindi wa tatu, sh.
100,000 kwa mshindi wa nne na tano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya
Spicenet, ambayo ndio wadhamini wa mchezo huo, Vinay Choudary alisema wameamua
kuungabnisha nguvu na chama cha Chess kuufufua mchezo huo Tanzania katika
jitihada za kuhakikisha nchi yetu inang’ara katika medani ya michezo katika
mashindano ya kimataifa.
“Nia yetu ni kukisaidia chama hiki kuhakikisha
mchezo huo unatangazwa na hatimaye kutambulishwa kwa watu wengi kupitia shule,
taasisi, vyuo vikuu na njia nyingine,” alisema.
Naye Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa
(BMT), Benson Chacha aliupongeza uongozi wa Chess pamoja na wadhamini wake kwa
kuamua kuurudisha mchezo huo ambao ulisajiliwa na BMT mwaka 1984.
“Sisi kama Baraza tutausaidia mchezo huu kupata
vitambulisho mbalimbali vya kushiriki mashindano ya mchezo huu, pia tunaomba
wadau wajitokeze kudhamini kwa lengo la kukuza michezo nchini,” alisema.