Shehata mwenye umri wa miaka 60, alifanikiwa ‘kuzitandika’ si chini ya timu nne zinazotarajiwa kuiwakilisha Afrika katika kombe la dunia wakati wa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika iliyofanyika mwezi wa kwanza nchini Angola na kutwaa ubingwa. Timu hizo ni Nigeria, Cameroon, Algeria na Ghana. Nigeria wao baada ya kumtimua kocha Shaibu Amodu, wakaamua kufuata hekima ya kutafuta maarifa toka kwa wapinzani wao ( if you can’t beat them, join them”) na kuonesha nia ya kumpa Shehata kazi hiyo yenye changamoto nzito. Hata hivyo inaonekana kuwa jitihada hizo zimekutana na ukuta mgumu wa Chama cha soka cha Misri.
Hakika si mengi tunayoweza kujifunza katika soka dhaifu la Nigeria wakati wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika na hatimaye kufukuzwa kwa Amoadu ukilinganisha na timu zingine zitakazoiwakilisha Afrika katika Kombe a Dunia. Ilichapwa na Misri, ikabahatika kwa Benin, ikapata ahueni kwa Msumbiji lakini ikawa dhaifu mbele ya Zambia na kulewa mbele ya Ghana. Hakika hatuwezi sema kuwa Soka la Nigeria wakati wa fainali hizo lilikuwa lenye uwezo wowote wa maana.
Picha-caption-Nigeria ilishika nafasi ya tatu lakini ikaamua kumtimua kocha
Nigeria wanaonekana kawaida kuanza vyema lakini hakika wanahitaji sana kuongeza msuli ili mambo yao yaweze kufanikiwa.
Kushindwa kufunga magoli lilikuwa tatizo wakati mwingine. Yakubu na Obafemi Martins walikosa magoli mengi. Lakini tatizo hasa ni kukosekana kwa kwa kiungo mchezeshaji Viungo wengi walioichezea Nigeria katika fainali hizo ni viungo wakabaji; John Obi Mikel, Dickson Etuhu, Sani Kaita na Yussuf Ayila, hali iliyosababisha mshambuliaji Osaze Odemwingie awe na kazi kubwa.
Nigeria wana tatizo jingine la kutocheza kama timu moja iliyoshikamana. Ni kikosi kilichojaa ubinafsi wa mchezaji mmoja mmoja. Hii itakuwa ni changamoto kubwa kwa kocha mpya hasa ukitilia maanani muda mfupi uliobaki kabla ya Fainali za Kombe la Dunia na timu pinzani katika kundi B ambazo ni Argentina, Korea ya Kusini na Ugiriki.
Wachambuzi wa soka kwa muda mrefu wamekuwa wakilisema jambo hilo kuhusu Nigeria lakini si kwa Ivory Coast.
Kama ilivyo kwa ndugu zao hao wa Afrika Magharibi, kikosi cha Ivory Coast nacho kilikosa kiungo mchezeshaji. Japo Yahya Toure na Didier Zokora ni viungo hodari lakini hawakuonesha kuelewana ipasavyo au uwezo wa kubadilisha mchezo. Jukumu hili linaonekana kuwaaangukia Abdulkader Keita na Bakary Kone, lakini kule Angola hawakuonesha la maana sana. Ukimtaja Gervinho, bado hakuweza kuonesha makeke licha ya matarajio makubwa aliyotwishwa.
Hiyo ni kwa upande wa ubunifu katika kiungo.Lakini udhaifu wake hatuwezi kuulinganisha na udhaifu mkubwa uliojionesha katika nafasi ya ulinzi hasa wakati wa kipigo cha nusu fainali toka kwa Algeria. Mabeki na viungo walipoteza kabisa maelewano, hali iliyojionesha wazi pale beki wa Algeria Madjid Boughera alipotumia vyema udhaifu huo kufunga goli la muhimu la kusawazisha katika dakika ya 92.
“Timu kubwa haziachii ushindi wa 2-1 upotee kirahisi kunapokuwa kumebaki dakika chache mechi kumalizika”, akasema kocha wa Ivory Coast kutoka Bosnia Vahid Halilhodzic. “Tulikuja na matumaini makubwa, lakini kwa mara nyingine Ivory oast imeshindwa kutoa matokeo mazuri. Si tatizo la kimwili ila ni la kisaikolojia”
Lilikuwa ni tatizo la kisaikolojia au ni matokeo ya pumziko refu la siku tisa lililosababishwa na kujiondoa kwa Togo? Wachambuzi wanaweza kusema ni tatizo la kisaikolojia, wakizingatia matokeo mabaya ya miaka ya nyuma. Mwaka 2006 Ivory Coast ilifungwa na Misri katika fainali, ikapoteza nusu fainali mwaka 2008 mbele ya hao hao Misri na mwaka huu ikabanwa mbavu na Algeria.
Inavyoonekana ni kuwa Ivory Coast hupata wakati mgumu ikikumbana timu zilizojipanga vyema. Sifa ambayo timu za Afrika Kaskazini wanayo. Lakini bora wajue kuwa wapinzani wao ndani ya kundi G, Korea ya Kaskazini, Ureno na Brazil, zote zina sifa hiyo hiyo ya kujiandaa na kujipanga vyema. La kutia hofu zaidi ni kwamba mashabiki wa Ivory Coast wanaonekana kupoteza imani yao kwa mshambuliaji Didier Drogba ambaye kiwango chake kule Angola kiliwakasirisha wengi.
Sina hakika kama watu wa Cameroun wana hisia na mawazo hayo hayo juu ya Samuel Eto’o. Lakini naye hakuwa katika kiwango chake kule Angola. Kocha Paul Le Guen alimchezesha nyuma ya washambuliaji wawili mbele katika kipigo cha robo fainali kutoka kwa Misri. Lakini kwa silika ya kiwindaji aliyo nayo Eto’o, inakuwaje achezeshwe katika nafasi hiyo?.
Kulikuwa na mengi ya kushangaza hasa ukitilia maanani matarajio mengi yaliyowekwa kwa viungo Stephane Mbia na Jean Makoun.
Lakini Mbia alipewa dakika 45 tu na Makoun akaachwa katika mechi dhidi ya Misri. Nafasi hizo wakachukua Enoh Eyong na George Mandjeck mwenye umri wa miaka 21, ambaye aling’ara katika pambano dhidi ya Misri.
“Niliamua kutia damu changa ili kuleta nguvu mpya” akasema kocha Le Guen. “Mechi yetu na Misri ilionesha nilikuwa sahihi”.
Hatimaye kulifanyika mabadiliko katika ulinzi. Rigobert Song hakuanzishwa na vijana wapya Nicolas N’Koulou na Aurelian Chedjou wakakamata nafasi.
Lakini Cameroun wana tatizo la kufungwa mapema. Misri wakaonesha udhaifu wa golikipa Carlos Kameni, licha ya kwamba kwa kawaida huwa huwa ni kizuizi imara golini lakini si kwa Ahmed Hassan.
Rahim Ayew na Hans Sarpei walicheza vyema Angola licha ya vikwazo kadhaa.
Cha kutia moyo ni kuwa wachezaji wote 19 (outfield players) walionja ladha ya kucheza soka Angola ambako mwinuko kutoka usawa wa bahari katika mji wa Lubango ni mita 1750. Hali hiyo itawaweka katika hali ya kukabili mechi za kundi E. Katika mwinuko wa jiji la Bloemfotein dhidi ya Japan ambao ni mita 1400 na dhidi ya Denmark jijini Petoria mita 1275. Mechi ya mwisho dhidi ya Uholanzi itakuwa ni katika usawa wa bahari.
Lakini kama kuna timu iliyofaidika na michuano ya Angola ni Ghana.Wachezaji wake sita wa kikosi cha kwanza walikosekana, wakiwemo wote wa nafasi ya kiungo na walinzi mahiri wawili. Vijana wachanga wa Ghana waliopata nafasi ya kucheza waliikabili michuano kwa ujasiri kiasi kwamba uzoefu huo unaweza kuwasaidia wakati wa kombe la dunia watakapokuwa wakikabiliana na wapinzani wao wa kundi D, Ujerumani , Australia na Serbia.
Hali ya kisaikolojia ya Ghana ilitiliwa mashaka hapo awali lakini vijana kama Kojo Asamoah, Samuel Inkoom, Agyemang Badu na Opoku Agyemang walionesha ujasiri mkubwa wa kuzikabili mechi ngumu na inaashiria hali nzuri ya siku za baadae kwa soka ya Ghana.
Timu ya Ghana imejengwa kutokana na kikosi cha vijana wa chini ya miaka 20 walionyakua kombe la dunia. Vijana sita kati ya walionza katika fainali dhidi ya Misri walikuwa na miaka 22 au chini. Lakini kwa kombe la Dunia inaweza isiwe rahisi kukamata nafasi ya kucheza. Hiyo ni kwa kuwa pia zile tofauti kati ya kocha Milovan Rajevac na Sulley Muntari zimemalizwa.
“Wanahitajika wachezaji wenye uzoefu kwa ajili ya kombe la Dunia.Tunao kama John Mensah, John Pantsil, Laryea Kingston, Michael Essien na Sulley Muntari. Wapo wengine pia” anasema kocha Milovan.
Baada ya michuano ya Angola, Milovan alilaumu ukosefu wa uzoefu kwa wachezaji wake lakini akasema kuwa anafurahia uzoefu waliopata vijana wale na kuamini kuwa utasaidia wakati wa kombe la dunia. Bila kuogopa kufanya maamuzi makubwa, kocha Milovan alionesha ubora wake pale timu ilipoweza kuingia fainali licha ya kuwa na majeruhi na changamoto nyingi.
Mafanikio yake makubwa ni kuweza kuwajenga wachezaji kucheza ki timu zaidi kuliko ilivyokuwa kwa timu zingine zitakazoiwakilisha Afrika katika Kombe a Dunia. Nani anajua mchango ambao ungetolewa na vijana wazoefu kama akina Essien, Muntari, Pantsil na wengine kama wangekuwa katika hali nzuri ya kuweza kucheza?
Kwa wengine wenye majina makubwa kama vile Drogba, Eto’o na Mikel ilikuwa ni hali ya kusikitisha. Je ni kwa sababu shauku ya kucheza katika kombe la mataifa ya Afrika kumezwa na aina ya maisha wanayoishi huko Ulaya? Au majina yao makubwa na hali ya soka Ulaya inaweza kuwa ndiyo sababu?
Kama siyo, je sababu ni nini? Lolote jibu liwalo naamini soka la Afrika katika fainali hizi za kombe la dunia litakuwa tofauti sana.