Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' akimnowa bondia Lulu Kayage wakati wa mazoezi yake ya kujiandaa na mpambano wake wa kugombania mkanda wa taifa desemba 25 na bondia Mwanne Haji mpambano utakaofanyika mkoa wa Morogoro katika uwanja wa jamuhuri picha na SUPER D BOXING NEWS |
BONDIA LULU KAYAGE |
Katika kipindi cha
hivi karibuni wamewika mabondia wengi sana nchini lakini kwa sasa
mabondia wanaotamba na kufanya vizuri wana hesabika ukiondoa kwa upande
wa wanaume bondia anaekuja juu zaidi kwa sasa kwa upande wa wanawake ni
Lulu Kayage
Bondia huyu aliye dhubutu kwa kumtwanga Winnie Mphahlele wa Afrika ya kusini mpambano uliofanyika Town
Hall, katika mji wa Limpopo, South Africa kwa T.K.O ya raundi ya tatu
kwenye mpambano wa raundi sita amekuwa tishio katika ukanda wa afrika na
anataka kudhilisha kuwa yeye ni zaidi ya mabondia wengine wa hapa nchini
akizungumza na mwandishi wa makala haya
bondia huyo kwa ajili ya kuelezea
maisha yake nje ya ulingo. Yafuatayo ni mahojiano hayo:
mwandishi, Unajihusisha na mchezo wa
ngumi ambao wengi wanaona ni wa kiume, je kama msichana ni changamoto gani
unakumbana nazo katika maisha?
Lulu: Kwa kawaida unapokuwa kwenye mchezo wa
masumbwi mtaani watu wengi wanakuogopa wanakuchukulia kama
mgomvi muda wowote unaweza kupigana na mtu lakini ni tofauti kwa
sababu ukishaingia huku hupigani hovyo. Changamoto nyingine mimi
nikiongea sauti yangu ya asili ni kubwa hivyo ninapokuwa kwenye
biashara zangu mtu anaweza akaja kununua kitu nikimjibu anaona naongea kwa
hasira wakati sio hivyo.
mwandishi: Ni kweli huwa mnakuwa wababe na wewe uliwahi kupigana na mtu
mtaani huku ukiwa bondia?
Lulu: Zamani nilikuwa napenda ugomvi na
mtu akinichoza nampiga kweli lakini tangu nimeanza mazoezi ya
ngumi hali hiyo iliondoka na kama kupigana najisikia raha nikiwa ulingoni ni
kupigana na bondia mwenzangu. Hata sasa akitokea mtu aseme tupigane
hadharani tofauti na mchezo naogopa na ninaweza kupigwa kwa kuwa
nitapigana kwa hofu ya kuwa ninayepigana naye nitamuumiza endapo
nitampiga sehemu mbaya kwa sababu uwezo wa kunipiga hana.
mwandishi: Familia inachukuliaje kazi unayofanya ya kupigana ngumi na wewe ni mtoto
wa kike?
Lulu: Wamepokea vizuri tu na wananiaunga mkono
kwa sasa lakini nilivyoanza niliwaficha na walifahamu kuwa nacheza ngumi baada
ya kuona picha yangu kwenye gazeti napigana wakashangaa na
kuniuliza imekuwaje nimeingia huko wakati wanajua mimi nafanya riadha.
mwandishi: Kama watu wanakuogopa rafiki zako wa karibu ni kina nani?
Lulu:Mimi marafiki zangu ni watoto wa kiume kwa
bahati mbaya au nzuri sina rafiki wa kike, ukiniona nimeongozana na msichana
ujue ndugu yangu. Sina mazoea na wasichana tangu nilipokuwa shuleni.
mwandishi: Kwa nini hupendi kuwa na marafiki wa kike?
Lulu: Wanawake mara nyingi wanakuwa na midomo
ya kuzungumza mambo ya watu yasiyowahusu sasa mimi sipendi. Hata
nyumba niliyopanga wanajua kama rafiki zangu wanaofika nyumbani kwangu ni
wavulana. Imefikia hadi wasichana wenyewe wanashindwa kunizoea hawajui
waanzie wapi kuwa na urafiki na mimi kwa sababu mambo ya kujadili
watu siayapendi lakini nikiwaona mahali wamekaa nawasalimia kama kawaida.
mwandishi: Kuna vitu vingine katika maisha lazima umshirkishe msichana mwenzako,
huwa unafanyaje wakati watu wako wa karibu wavulana?
Lulu: Nikihitaji ushauri au vitu
vinavyohusu msichana huwa nawashirikisha wasichana ambao ni ndugu zangu.
mwandishi: Mara nyingi mavazi yako huwa kama ya kiume, je hiyo inatokana na unavyokaa
karibu nao?
Lulu: Nahisi hivyo kwa sababu siku nikivaa
gauni sijui kuna nini sio rahisi. Lakini Kikubwa kilichochangia
kupenda mavazi haya ni kwa sababu nimelelewa na baba tangu nikiwa na
miezi mitano baada ya mama yangu kufariki. Unajua mwanaume anavyolea
mtoto huwa hamvalishi sketi kutokana na mazingira na ikawa nikivalishwa sketi
nalia kutwa nzima hata nilivyoanza shule nguo niliyoshonewa juu
sketi ndani imetengenezwa kama suluari
mwandishi: Umeolewa, una mchumba au unaishi na nani?
Lulu: Sijaolewa na wala sina mchumba, ninaishi
mwenyewe.
mwandishi: Kwa nini au ndio hivyo wanakuogopa?
Lulu: Nadhani muda bado haujafika na wapo
wanaonifuata nakataa kwa sababu wengi ni vijana ambao siwaelewi kwa kuwa
haiwezekani mtu aje amevaa suluari mlegezo halafu nimkubali. Mimi navaa suluari
lakini sipendi mtu anaevaa mlegezo.
mwandishi: Maisha ya kuishi msichana peke yake yana changamoto gani?
Lulu: Binafsi nayaona ni mazuri kwa kuwa napenda
kujishughulisha na kazi. Nilikuja mjini nikiwa mdogo nikitokea Iringa na
kufanya kazi za ndani kwa miaka miwili bila malipo.
mwandishi: Uliwezaje kufanya kazi bila malipo na ulikuja kulipwa fedha zako baadaye?
Lulu: Nilikuja kuondoka, bahati nzuri mama
niliyekuwa naishi naye alikua anafuga ng’ombe akawa ananipa maziwa nauza
hivyo nikawa napata hela kidogo ambazo nabakisha sokoni nikafungua
akaunti benki nikawa naweka hadi nikafikisha 600,000 nikaondoka
nikatafuta chumba. Kutokana na utoto nilipata shida kupata kwa kuwa kila ninapokwenda
kwa mwenye nyumba ananikataa hadi nikatafuta msaada polisi wakaniasaidia.
mwandishi: Ilikuwaje ukaingia kwenye ngumi?
Lulu: Ni mchezo niliokuwa naupenda, kwa kuwa
nilikuwa nafanya mazoezi ya riadha nikakutana na kijana mmoja anaitwa Omari Bai nikamuuliza
wapi wanafundisha ngumi akanipeleka kwa mzee Habibu Kinyogoli 'Masta'.
mwandishi: Unafanya mazoezi mara ngapi kwa siku?
Lulu: Mazoezi nafanya mara mbili.
mwandishi: Unapendelea chakula gani?
Lulu: Napenda ugali maharage na mboga za majani
na asubuhi napendelea kula matunda.
mwandishi: Kitu gani kinakuongezea kipato?
Lulu: Nafanya biashara ya matunda. Nina genge
langu la kuuza matunda lipo maeneo ya Mkwajuni, Kinondoni.
mwandishi: Kuna vishawishi vingi kwa vijana kama vile matumizi ya dawa za kulevya
hasa ukiwa kwenye michezo, wewe unajizuaje?
Lulu: Namshukuru Mungu malezi ya baba
yamenilinda kwa kuwa sijawahi kumuona akivuta sigara, kunywa pombe au kuingiza
mwanamke ndani hivyo ni ngumu mimi kufanya vitu hivyo. Nikiwa na rafiki
anatumia vitu hivyo naepukana naye.Bondia huyo kwa sasa anasimamiwa mapambano yake ya ndani na nje ya nchi na kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa mchezo wa masumbwi nchini
No comments :
Post a Comment