Msanii John Makanyaga (Mchungaji) 'Mr Bomba' enzi za uhai wake |
Moja ya kazi za mwisho mwisho za marehemu Mr Bomba |
MWILI wa msanii nyota wa zamani wa Kaole Sanaa, John Makanyanga maarufu kama Mr Bomba unatarajiwa kuagwa kesho jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa Mpwapwani, Dodoma kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya Jumanne.
Kwa mujibu wa mmoja wa wasanii wenzake ambaye hivi karibuni walitoka na filamu mpya iitwayo 'Dangerous Deal', Adam Malele 'Swebe Santana' ni kwamba mwili wa msanii huyo aliyerafiki jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili utaagwa kesho Jumatatu kabla ya kusafirishwa jioni kuepekwa Mpwapwa.
Swebe, ambaye anayemlilia Mr Bomba na kudai ni mtu aliyekuwa naye karibu tangu wakiwa wote Kaole, alisema mwili huo utaagwa nyumbani kwa marehemu Buguruni Malapa karibu na Kanisa la Anglikana, jijini Dar.
"Kwa taarifa ambazo mpaka muda huu nilizonazo ni kwamba marehemu ataagwa kesho kabla ya kusafirishwa kwao Mpwapwa Dodoma kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika siku ijayofuata," alisema.
Mr Bomba, ambaye kitaaluma alikuwa ni mwalimu aliyewahi kufundisha Shule ya Sekondari Makongo na nyingine binafsi eneo la Mbezi, alifariki jana baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na kansa ya uvimbe wa kwenye ini mbali na sanaa na ualimu pia alikuwa Mtumishi wa Mungu akiwa kama Mchungaji wa Kanisa la Anglikana.
Enzi za uhai wake msanii huyo aliyejaliwa mwili mkubwa alitamba na tamthilia mbalimbali akiwa na kundi la Kaole Sanaa iliyokuwa ikirushwa na kituo cha ITV, akimudu zaidi nafasi ya 'kibosile' na wakati mwingine kama 'mafia' anayehusika na biashara ya dawa za kulevya na alicheza filamu kadhaa ikiwamo 'Kidole Tumbo', iliyozuiwa kuingizwa sokoni.
Mbali na uigizaji, pia marewhemu alikuwa mtunzi, mwandishi wa miswada ya filamu na kazi ya karibu kuiandaa ni Dangerous Deal ambayo aliitunga na kuiandikia mswada mwenyewe na kuongoza na Swebe ambapo mbali na kuichezea yeye mwenyewe, pia aliigiza na Swebe, Chuchu Hans, Hashim Kambi, Sebastian Mwanangulo, Mama Sonia na wengine.
Mungu aiweke mahali pema roho ya marehemu Mr Bomba.
No comments :
Post a Comment