ZIKIWA
zimebaki siku chache kabla ya mradi wa mabasi yaendayo kasi kuanza,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa taasisi zinazohusika na
utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili
kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
“Katika
kipindi hiki cha majaribio, ambacho madereva wameanza kutumia barabara
za BRT, hakikisheni mnatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu namna ya
kuvuka barabara, kuzuia wenye bodaboda kutumia barabara hizo kuelezea
na matumizi ya taa za barabarani kwa madereva wote,” amesema.
Ametoa
agizo hilo jana usiku (Ijumaa, Aprili 15, 2016) wakati akizungumza na
wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao
alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu aliwataka watendaji wa wakuu wa taasisi wahakikishe wanapanua wigo
na kutumia vyombo vya habari vingi kadri iwezekanavyo pamoja na
mitandao ya kijamii katika kuelimisha raia juu ya zoezi hilo.
Akifafanua
kuhusu hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa
TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema miundombinu kwa ajili ya
mradi huo imekamilika na usafiri huo utaanza hivi karibuni.
Mhandisi
huyo ametumia fursa huyo kutoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu ya
barabara hizo kwa sababu imeigharimu Serikali fedha nyingi.
Naye
Mrakibu wa Polisi (SP), John Shawa kutoka Makao Mkuu ya Trafiki alisema
kuanzia kesho zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka litaanza
hivyo amewaomba wananchi kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama
barabarani.
"Kuanzia
kesho linapoanza zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka ni vema
watu wakatumia vizuri barabara hasa madereva wa bodaboda na madereva
wengine watambue kuwa hawaruhusiwi kupita katika barabara hizo,"
alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAMOSI, APRILI 16, 2016.
No comments :
Post a Comment