Afisa Habari wa Kitengo cha
Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama akizungumza na
wanafunzi wa shule ya msingi ya Diamond juu ya umuhimu wa kujifunza
mauaji ya kimbari ya wayahudi ya mwaka 1933.
Na Mwandishi Wetu, MOblog Tanzania
Kitengo cha Habari cha Umoja wa
Mataifa (UNIC) kimeendelea kutoa mafunzo na elimu juu ya umuhimu wa
kukumbuka maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya ukombozi wa kambi za
mateso ya Auschwitz kwa wanafunzi wa sekondari na shule za msingi
nchini.
Akizungumza na wanafunzi wa
shule ya msingi ya Diamond ya jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Afisa
habari wa kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma
Ledama amesema kwamba ni muhimu kwa kizazi na kizazi kujifunza madhara
ya mauaji na maangamizi ya moto dhidi ya wayahudi yaliofanywa na askari
wa kinazi wa Ujerumani.
“Ni muhimu kutoa mafunzo kwa
vijana wakitanzania wa shule za msingi na sekondari ili wajue kwamba
tofauti za rangi na za kidini hazina nafasi ya kutugawa kama binadamu,”
amesema Nkhoma.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Diamond na Mlezi wao wakimsikiliza Bi. Ledama (hayupo pichani).
Afisa Habari wa Kitengo cha
Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama, akisoma ujumbe
wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataiafa katika siku ya kimataifa ya
maadhimisho ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji ya maangamizi ya moto.
Alisisitiza kwamba mauaji na
mateso ya Auschwitz yalipoteza mamilioni ya watu wasio na hatia na
mafunzo haya yanaonyesha chuki na ubaguzi dhidi ya wayahudi na chuki za
aina nyingine yoyote hazina nafasi katika ulimwengu wa leo.
Nkhoma amesema kwamba binadamu
wote ni sawa na tofauti za kipato au dini au rangi haziwezi tena kujenga
chuki dhidi ya binadamu wengine kwa sababu wote kama binadamu tuna haki
sawa mbele za mungu.
Wanafunzi wa shule ya msingi ya
Diamond jijini Dar es Salaam, wakifuatilia sinema maalum ya mauaji ya
kambi za mateso ya wayahudi mwaka 1933.
Wakati huo huo, ujumbe wa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika siku ya kimataifa ya maadhimisho ya
kuwakumbuka wahanga wa mauaji ya maangamizi ya moto amesema aliona
makambi ambako wayahudi, waroma, wasinti, mashoga, wafungwa wa kivita na
watu wenye ulemavu walitumia siku za mwisho katika hali ya kinyama.
“Umoja wa Mataifa ulianzishwa
kuzuia kila aina hii ya fazaa kutokea tena, lakini bado misiba kuanzia
Cambodia hadi Rwanda mpaka Srebrenica inaonyesha kuwa sumu ya mauaji ya
kimbari bado inatiririka,” ilisema taarifa hiyo.
Pichani juu na chini ni Wanafunzi wa shule ya msingi ya Diamond wakisoma baadhi ya machapisho ya Umoja wa Mataifa.
No comments :
Post a Comment