Shirika la Majisafi
na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), imetangaza kuwako na ongezeko la Maji
katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam, pamoja na maeneo ya miji ya
Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani, baada ya mtambo wa Maji wa Ruvu chini kuanza
kufanya majaribio ya uzalishaji wa Maji .
Akiongea na waandishi
wa habari kaimu meneja uhusiano wa DAWASCO, Bi. Everlasting Lyaro, amesema kuwa
kutokana na ongezeko hilo la Maji watu wengi wameanza kupata huduma ya
Majisafi, na pia kumekuwepo na ongezeko la uvujaji wa Maji katika maeneo mengi
ya jiji la Dar es salaam, hasa katika maeneo ambayo yalikuwa na miundombinu ya
Maji lakini hayakuwa na huduma ya Maji na baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa yakipata
Maji kwa msukumo mdogo (Low pressure)
“Kufuatia
ongezeko hili la Maji watu wengi wameanza kupata huduma ya Majisafi, na uvujaji
wa Maji umeongezeka katika maeneo ambayo aidha yalikuwa na miundombinu ya Maji
lakini hayakuwa na huduma ya Maji au maeneo ambayo yalikuwa yakipata Maji kwa
msukumo mdogo” Alisema Bi. Lyaro
Aidha, ametoa wito
kwa wateja na wananchi wote kutoa taarifa za uvujaji huo wa Maji pindi
wanapobaini kuwapo na uvujaji wa Maji katika makazi yao na maeneo mbalimbali ya
jiji kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa kupiga simu namba 022194800 au
0800110064 (Bure).
“Namba hizi ziko wazi
saa 24 kwa siku na mteja hatakatwa gharama yoyote akipiga simu hizi. Hivyo
tunaomba wateja wetu waisaidie Dawasco kupunguza upotevu wa maji kwa kutupa
taarifa za mivujo na kupasuka kwa mabomba” alisema bi Lyaro.
Kutokana na ongezeko
hilo la Maji maeneo yaliyoanza kupata Maji baada ya majaribio ya mtambo huo
kuwa ni Tandale,Manzese makunimula,Mwananyamala,Kinondoni mkwajuni, baadhi ya
maeneo ya vingunguti,changombe,ubungo-mabibo na city centre.
Pia, DAWASCO imetumia
nafasi hiyo kuwakumbusha wateja wote kulipia huduma ya Maji kwa wakati kwani
watu wengi kwa sasa wameanza kupata huduma ya Majisafi na salama kutokana na
kuongezeka kwa uzalishaji wa Maji katika mtambo wa Maji wa Ruvu chini, hivyo
hawana budi kuyalipia ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma ya Maji.
Kuongezeka kwa huduma
ya Maji katika jiji la Dar es salaam na Mji wa Bagamoyo kumetokana na kukamilika upanuzi wa mtambo wa
Ruvu chini ulioanza mwaka 2011 hivyo kuongezeka kiasi cha uzalishaji wa Maji
kutoka wastani wa lita milioni 182 hadi lita 270 kwa sasa.
No comments :
Post a Comment