Priscus Nyoni akijiandaa kuingiza mpira katika shimo wakati wa mashindano ya gofu ya Zain Lugalo Fiddle yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika uwanja wa TPDF Lugalo jijini Dar es Salaam .
Priscus Nyoni amefanikiwa kuwa mshindi katika mashindano ya mchezo wa gofu yaliyofanyika juzi katika viwanja vya mchezo huo vya Lugalo jijini Dar es Salaam baada ya kupata pointi 31.
Nyoni aliyekuwa akichuana vikali na Terence Mwakaliku alifanikiwa kumshinda kwa tofauti ya pointi 2 baada ya mpinzani wake kujipatia pointi 29.Ushindi huo ulimpatia Nyoni zawadi mbalimbali kutoka Zain ikiwemo seti ya vyombo vya ndani.
Nyoni alisema kuwa zawadi aliyoipata itakuwa changamoto kwake ili azidi kufanya vizuri katika mashindano ya mchezo huo yatakayofanyika wiki ijayo.
“Zawadi hii kwangu ni changamoto kubwa kwasababu kama nimeweza kuipata leo sitaki kuikosa tena,” alisema Nyoni
Nyoni ambaye ni mchezaji kijana wa gofu alisema kuwa hakuamini kama atashinda kwani mchezo ulikuwa mgumu na upinzani mkali na kusema kuwa siri ya mafanikio ni kufanya mazoezi kwa bidii.
Mbali na Nyoni washindi wengine ni Terence Mwakaliku , Simon Sayore na Stephania Sayore. Washindi hawa pia walijipatia zawadi mbalimbali ikiwemo miavuli,vyombo vya nyumbani pamoja na muda wa maongozi vyote kutoka Zain.
Michuano hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kila mwisho wa wiki chini ya udhamini wa Kampuni ya simu za mkononi ya Zain itaendelea wiki ijayo katika viwanja hivyo kwa kuwashirikisha wachezaji wa rika mbalimbali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
No comments :
Post a Comment