Ni mara ya tatu kufuzu fainali, lakini bado hawajapata kushinda Kombe la Dunia.
Uholanzi inapania kupiga hatua moja zaidi na kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, licha ya kucheza fainali mara mbili.
Mabao mawili yaliyofungwa katika muda wa dakika tatu kipindi cha pili na Wesley Sneijder na Arjen Robben yaliisaidia Uholanzi kuishinda Uruguay na kuingia fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1978.
Giovanni van Bronckhorst alikuwa ameifungia Uholanzi bao la mapema, lakini Diego Forlan akaisawazishia Uruguay kwa shuti la mbali muda mfupi kabla ya mapumziko.
Katika muda wa majeruhi Uholanzi walijikuta kwenye hatari ya ushindi kuwaponyoka wakati Maxi Pereira alipofunga bao la pili la Uruguay, lakini mchezo ukamalizikia hapo.
Kabla ya mwaka 1978 Uholanzi ilikuwa imecheza fainali ya mwaka 1974 mjini Munich ambapo ilishindwa na Ujerumani 2-1.
Mwaka 1978 Uholanzi walishindwa kwenye fainali na wenyeji Argentina mabao 3-1 mjini Buenos Aires.
Fainali ya Jumapili itakuwa ya tatu kwa Uholanzi, na mshambuliaji wa Liverpool, Dirk Kuyt anasema anaamini wakati umewadia kutwaa Kombe hilo baada ya 'kulinusa' mara mbili.
No comments :
Post a Comment