Ujerumani imeiadhibu Argentina kwa kuifunga mabao 4-0 kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia katika uwanja wa Green Point mjini Cape Town na kujipatia nafasi katika nusu fainali.
Juhudi za Ujerumani kutaka kufuzu miongoni mwa nne bora zilianza katika dakika ya tatu wakati Thomas Muller alipofunga kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Bastian Schweinsteiger.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Ujerumani wakiongoza 1-0 na katika dakika ya 68, Miroslav Klose akiichezea nchi yake mechi ya 100 aliongeza bao la pili kukamilisha pasi ya Lukas Podolski.
Podolski aliendelea kupenyeza pasi za kupendeza kutokea upande wa kushoto, na katika dakika ya 74 alitoa moja ambayo mlinzi Arne Friedrich alifunga bila matatizo, na kuipatia Ujerumani bao la 3.
Klose alipata fursa nyingine katika dakika ya 89 kumalizia pasi nyingine kutoka Podolski na kuandikisha bao lake la pili, na la nne kwa Ujerumani.
Uhasama
Katika mashindano ya Kombe la Dunia yaliyopita timu hizo mbili zilikutakana katika hatua ya robo fainali ambapo Ujerumani walishinda kupitia mikwaju ya penati.
Kwenye mechi ya Jumamosi, Ujerumani waliwavuta Argentina upande wao mara kwa mara kisha kuwavamia haraka, mkakati ambao uliwawezesha kupata ushindi mkubwa.
Walinzi wa Ujerumani walimdhibiti nyota wa Argentina Lionel Messi ambaye aliweka juhudi nyingi za kutaka kurudisha goli kwa mikwaju ya mbali.
Sasa Ujerumani inatarajia kuchuana kwenye nusu fainali na mshindi kati ya Uhispania na Paraguay.
Miroslav Klose anahitaji kufunga mabao mawili tu kwenye michuano iliyosalia ili kuwa mchezaji anayeongoza kwa ufungaji wa mabao mengi katika historia ya michuano ya Kombe la Dunia. Kwa sasa analingana na Gerd Muller pia wa Ujerumani ambaye amefunga magoli 14, anayeshikilia rekodi ni Ronaldo wa Brazil akiwa na magoli 15.
No comments :
Post a Comment