Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akilihutubia Bunge mjini Dodoma leo.
Rais Jakaya Kikwete akiendelea kulihutubia Bunge..........
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Mohammed Gharib
Bilal,akiwasili katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo kusikiliza
Hotuba ya Rais.
************************************************
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili
niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu
kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa
kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja
kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki
chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni
Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja
kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia
waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania
katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo
si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni
kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania
katika Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo
niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni
vyema nifanye hivyo.
Kuhusu
mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri
katika utekelezaji wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya
wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya
Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba. Kinachosubiriwa
kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa
kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka
kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua
zinazofuata. Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na
pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya
Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge
Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na
kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika
Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata
Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na
tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika
kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa
sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa
maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao
umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli
hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
No comments :
Post a Comment