Mshambuliaji
wa Simba Betram Mwombeki, akidhibitiwa na beki wa Ashant United, Tumba
Sued, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliochezwa leo jioni
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo Simba
imeibuka na ushindi wa mabao 4-2 na kufikisha jumla ya Pointi 24
wakiendelea kubaki nyuma ya watani wao wa Jadi Yanga kwa tofauti ya
Pointi 1.
Mshambuliaji
wa Simba,Amis Tambwe,akijiandaakupiga shuti mbele ya beki wa Ashant
United, Jaffari Gonga,wakati wamchezo huo. Picha na Habari Mseto
**********************************
**********************************
KOCHA
Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni leo ameshusha presha ya kutaka
kung’olewa katika klabu hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2
dhidi ya Ashanti United katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Ikitoka
kutoa sare tatu dhidi ya Yanga (3-3), Coastal Union (0-0) na Kagera
Sugar (1-1) na kufungwa 2-1 na Azam, Simba SC leo ilipata ushindi wake
kupitia kwa Betram Mwombeki, aliyefunga mawili, Amisi Tambwe na
Ramadhani Singano ‘Messi’.
Pamoja
na ushindi huo, Simba SC inabaki nafasi ya nne kwa pointi zake 24,
baada ya kucheza mechi zote 13 za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Azam
na Mbeya City zenyewe zina pointi 26 kila moja na Yanga inafuatia ikiwa
na pointi zake 25, ambapo timu zote hizo zinashuka dimbani kucheza
mechi zake za mwisho kesho.
Simba
SC walitangulia kupata bao katika dakika ya nane kupitia kwa winga wake
machachari, Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyepasua katikati ya ukuta wa
Ashanti baada ya pasi ya Amisi Tambwe kabla ya kumchambua kipa mkongwe,
Amani Simba.
Ashanti
walisawazisha dakika ya 45 mfungaji, Hussein Swedi aliyeunganisha kwa
kichwa krosi maridadi ya Hussein Mkongo kutoka wingi ya kulia.
Timu hizo
zilishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza, Ashanti wakigonga pasi fupi
fupi zenye kusisimua na Simba wakitumia mipira mirefu kushambulia
kupitia kwa washambuliaji wake wawili, Tambwe na Betram Mombeki.
Kipindi cha pili,
mabadiliko yaliyofanywa na Kocha mkongwe, Alhaj Abdallah Athumani Seif
‘King Kibadeni’ kuwatoa wakongwe Henry Joseph na Amri Kiemba na
kuwaingiza chipukizi Said Ndemla na William Lucian ‘Gallas’ yaliisaidia
Simba kupata ushindi.
Amisi Tambwe
alifunga bao la pili dakika ya 46 tu akipokea pasi ya Singano ‘Messi’ na
Mombeki akafunga la tatu dakika ya 50, akiunganisha krosi ya Haruna
Shamte.
Mkongwe Said
Maulid ‘SMG’ aliifungia Ashanti bao la pili dakika ya 53 kwa pasi ya
Hussein Swedi, lakini Mombeki akaihakikishia Simba SC ushindi kwa bao
zuri dakika ya 61 akiunganisha krosi ya Shamte tena.
Simba SC ingepeta
mabao zaidi kama ingeweza kutumia nafasi zaidi ya mbili nzuri
ilizotengeneza. Kipa Amani Simba alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika
ya 90 baada ya kudakia nje ya eneo lake mpira. Nahodha Paul Maona alimpisha kipa Daudi Mwasongwe akamalizie mchezo.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa;
Abuu Hashimu, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Gilbert Kaze,
Hassan Hatibu/Hassan Isihaka dk75, Jonas Mkude, Ramadhani Singano
‘Messi’, Henry Joseph/Said Ndemla dk46, Betram Mombeki, Amisi Tambwe na
Amri Kiemba/William Lucian dk46.
Ashanti United;
Amani Simba, Hussein Mkongo, Jaffar Gonga, Tumba Swedi, Samir Ruhava,
Iddi Said, Fakih Hakika, Paul Maona/Daudi Mwasongwe dk90, Hussein Swedi,
Said Maulid ‘SMG’/Abdul Kimbirwa dk83 na Joseph Mahundi.
No comments :
Post a Comment