BENDI
za Twanga Pepeta, Msondo Ngoma na wanamuziki kibao kutoka Sikinde ni
sehemu ya wasanii watakaosindikiza tamasha kubwa la Gurumo 53
litakalofanyika mwezi huu.
Tamasha
hilo ambalo ni mahsusi kwa ajili ya kumuaga mwimbaji mkongwe Muhidin
Maalim Gurumo litafanyika Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya TCC
Club Chang’ombe Jumamosi ya Desemba 14 mwaka huu.
Kwa
mujibu wa kamati ya watu sita inayoratibu tamasha hilo, Gurumo anaagwa
baada ya kutangaza rasmi kuachana na muziki wa jukwaani baada ya kudumu
kwenye kazi hiyo kwa miaka 53.
Mratibu wa kamati hiyo Juma Mbizo amesema kutakuwa pia na wasanii wa bongo fleva, vichekesho na sarakasi.
Aidha Mbizo amesema tamasha litatanguliwa na bonanza la soka la maveterani.
Hadi
kustaafu kwake Gurumo aliyezitumikia pia bendi za Kilimanjaro Chacha,
Rufiji Jazz, Kilwa Jazz, Sikinde na OSS – Ndekule, alikuwa ni kiongozi
na mmoja wa wamiliki wa Msondo Ngoma ambayo hapo awali ilijulikana kwa
majina ya NUTTA, Juwata na OTTU. Gurumo ameitumika Msondo katika majina
yote ya nyuma.
Wasanii
waliowahi kuitumikia Sikinde ambao watakuwepo kumsindikiza Gurumo ni
pamoja na Cosmas Chidumule, Abdallah Gama, Hussein Jumbe, Mashaka
Shaaban, Kalamazoo, Henry Mkanyia na Karama Legesu. Wengine ni Ali
Yahaya na Boniface Kachala, Benno Villa Anton, Tshimanga Kalala Assossa
na Ibrahim Mwinchande.
Baadhi ya wasanii wengine watakaotumbuiza ni Komandoo Hamza Kalala, Kassim Mapili, Hafsa Kazinja na Waziri Ali.
Kamati
ya Gurumo iko chini ya uenyekiti wa Asha Baraka, makamu ni Waziri Ali
na katibu ni Said Mdoe huku mratibu akiwa Juma Mbizo, wajumbe ni Said
Kibiriti na Richardson Sakala.
No comments :
Post a Comment