Steve Nyerere |
Steve Nyerere alipochanguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bongo Movie akiwa na viongozi wenzake kabla ya kujiuzulu hivi karibuni |
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Bongo Movie, Steve Nyerere amefichua kilichomkimbiza kwa kujiuzulu katika Umoja huo wa Waigizaji wa filamu.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Steve Nyerere ambaye majina yake kamili ni Steven Mengele alisema, misimamo yake ya kutetea na kujenga nidhamu katika umoja huo sambamba na kuweka mizani sawa kwa wasanii wanachama ndicho kilichomponza, mbali na tofauti za kiitikadi za kisiasa baina yake na viongozi wenzake.
Steve Nyerere alisema baadhi ya viongozi wenzake walikuwa wakimuona kama alikuwa akiitumia Bongo Movie kujijenga kisiasa, bila kujua umaarufu wake kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa wameisaidia Bongo Movie kuwaomboleza na kuwazika wasanii wenzao bila ya aibu licha ya umoja huo kutokuwa na fedha.
"Unajua nilikuwa najenga nidhamu na kutaka kila mwanachama kujiona sawa ndani ya Bongo Movie, hilo halikuwapendeza wenzangu na kuanzisha majungu, wakati naingia hakukuwa na akaunti wala fedha, lakini tumeweza kuwazika bila ya kutia aibu wenzetu, Rachel Haule 'Recho', Adam Kuambiana na George Otieno 'Tyson," alisema.
Muigizaji huyo alisema licha ya kujivua uenyekiti, bado anaendelea kuwa mwanachama muaminifu wa Bongo Movie na kuwa tayari kujitolea kwa jambo lolote, licha ya kukiri kwamba ni vigumu kuondoa itikadi zake kwa CCM, kama ambavyo hawezi kumuingilia Prof Jay ambaye ni rafiki yake kwa uaminifu na mapenzi yake kwa CHADEMA.
"Ni mambo madogo madogo ambayo wenzangu wameshindwa kuyavumilia kwa sababu ya kiitikadi na misimamo ya kuwajali hata wasanii chipukizi mradi ni wanachama wa Bongo Movie, lengo likiwa kujenga misingi imara ya kundi hilo hata wale wazoefu watakapokuwa wameachana na fani hiyo," alisisitiza.
Steve Nyerere alisema yeye atakuwa tayari kutoa ushauri na mambo mengine ya maendeleo hata akiwa nje ya uongozi kwa nia ya kuhakikisha Bongo Movie inafika mbele na katu hana kinyongo na yeyote.
No comments :
Post a Comment