Shirikisho la soka Tanzania (TFF) jana lilitangaza sifa nane za msingi ambazo kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars, anatakiwa awe nazo.
TFF imefikia maamuzi hayo baada ya wajumbe wa kamati ya utendaji wa shirikisho hilo kukutana wiki iliyopita na kukubaliana sifa ambazo mrithi wa Mbrazili, Marcio Maximo, anatakiwa awe nazo.
Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alisema jana kuwa kocha mpya ajaye anatakiwa awe na kiwango cha elimu kuanzia ya sekondari, uwezo wa kuzungumza, kusoma na kuandika Kiingereza, na awe elimu ya kiwango cha kuanzia diploma ya kufundisha soka kutoka katika chuo kinachotambulika. Na sifa ya ziada, awe na leseni ya ualimu wa soka inayotambulika kimataifa. Mwakalebela alitaja sifa nyingine kuwa ni awe na cheti cha ukufunzi wa makocha wa soka, umri kuanzia miaka 30 na pia awe na uzoefu usiopungua miaka mitano wa kufundisha timu za daraja la juu (timu za taifa ni sifa ya ziada).
Alisema pia rekodi nzuri ya kufundisha katika nchi zinazoendelea ni sifa ya ziada ya kocha huyo anayetaka kutuma maombi yake, huku sifa nyingine ikiwa ni kuwa mwadilifu na mwenye haiba.
"Pia awe na uwezo wa kuwasiliana na wasaidizi wake na wakuu wake wa kazi," alisema katibu huyo.
Aliongeza kuwa sifa nyingine ya kocha huyo mpya ni lazima awe na uwezo wa kutumia kinakilishi (kompyuta) na programu za kisasa.
Mwakalebela alisema pia ni lazima kocha huyo awe na maarifa ya kuongoza jopo la ufundi na mbinu za kisasa za ufundishaji wa mchezo huo.
Alisema kwamba makocha wote wanaotaka ajira hiyo mpya wanatakiwa kuanza sasa kutuma maombi yao na mwisho ya kufanya hivyo ni Februari 28. “Waombaji watume maombi yao kwa katibu mkuu wa TFF,” alisema.
Alisema kocha huyo atakuwa na majukumu ya kuandaa programu za muda mrefu, kati na fupi kulingana na mashindano yanayomkabili huku akilinda nidhamu ya wachezaji.
Kocha huyo mpya pia atakuwa na jukumu la kuendesha mafunzo ya ualimu wa mchezo huo hapa nchini pale atakapopangiwa kufanya hivyo huku pia akitakiwa kuwa karibu na makocha wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Daraja la Kwanza.
RAIS DKT.SAMIA SULUHU HASSAN ATOA POLE AJALI YA KARIAKOO
-
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
akitoa salamu za pole kwa waathirika wa ajali ya kudondokewa na gorofa
Kariakoo Jij...
6 days ago
No comments :
Post a Comment