Ilikuwa ni fahari kwa Kenya siku ya Jumapili wakati wanariadha wake wawili walipoweza kutwaa ushindi katika mashindano ya Great North Run, mjini Gateshead, Uingereza, wakati Martin Mathathi alipomaliza wa kwanza na akiandikisha rekodi, huku kwa upande wa kina dada, mwanariadha mwenzake kutoka Kenya, Lucy Karbuu alimaliza katika nafasi ya kwanza pia, na akiwa wa tatu kuwahi kwenda kasi zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Martin Mathathi aliandikisha muda wa kasi zaidi katika historia ya mashindano hayo kwa kumaliza katika muda wa dakika 58, sekunde 56.
Karbuu aliwashangaza wengi kwa muda alioandikisha, akimaliza mbio hizo katika muda wa saa moja, dakika saba na sekunde sita, huku Mreno Jessica Augusto akishikilia nafasi ya pili.
Wanariadha wawili wa Uingereza, Jo Pavey na Helen Clitheroe waliyatumia mashindano hayo katika kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 mjini London, Olympics.
Pavey, mwenye umri wa miaka 37, alimaliza katika nafasi ya nne, huku Clitheroe akifuata katika nafasi ya tano.
Mathathi, ambaye alishinda medali ya shaba mita 10,000 katika mashindano ya dunia ya mwaka 2007 mjini Osaka, Japan, alifanikiwa kupunguza sekunde tisa katika rekodi ya Zersenay Tadese wa Ethiopia, iliyoandikishwa mwaka 2005, ya muda wa dakika 59, sekunde 5.
Huo ni kati ya muda bora zaidi, miongoni mwa sita bora, kuwahi kuandikishwa katika mashindano ya nusu-marathon.
Mkenya Jonathan Maiyo alijitahidi kutimka na kuwatangulia wenzake baada ya maili tano za mashindano, lakini kufikia maili nane, Mathathi alikuwa tayari ameshampita.
No comments :
Post a Comment