Na Ismail Ngayonga
Maelezo
Dar es Salaam
WATANZANIA na wadau wa maendeleo nchini wamehimizwa kujitokeza na kuwekeza katika vivutio vilivyopo badala ya fursa hizo kuwaachia wageni kutoka nje ya nchi.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano wa uwekezaji katika ukanda wa ziwa Tanganyika unaotajiwa kufanyika tarehe 17 oktoba mwaka huu.
Mhandisi Manyanya alisema wakati umefika kwa Watanzania kujitokeza na kuwa vinara katika sekta ya uwekezaji na kamwe wasitishwe na suala la uwezo, kwani katika mipango iliyopo inawasaidia pia wenye uwezo mdogo wa kuwekeza.
“Mikoa iliyopo katika ukanda wa ziwa Tanganyika ambayo ni Kigoma, Rukwa na Katavi ina fursa nyingi za uwekezaji, hivyo kila Mtanzania anahimizwa kuwekeza hata kama ana uwezo mdogo kifedha yapo baadhi ya maeneo unayoweza kuwekeza” Alisema Mhandisi Manyanya.
Alisema mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ni miongoni mwa mikoa yenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa ukanda huo wadau wote wa ndani na nje ya nchi wana fursa sawa ya uwekezaji kupitia mipango iliyopo.
Manyanya alisema kwa muda mrefu ukanda wa ziwa Tanganyika tangu enzi ya ukoloni umesifika kwa miundombinu duni ya huduma za kiuchumi na kijamii, hatua hiyo iliyosababisha mikoa yake kusahaulika katika harakati za maendeleo ya mawasiliano ya barabara, usafiri wa majini, reli, usafiri wa ndege pamoja na mawasiliano ya simu, runinga na redio.
Aliongeza kwa kutambua changamoto hizo, Serikali ya awamu ya nne imefanya kazi kubwa katika kufungua ukanda huo kwa kujenga miundombinu ya barabara za lami, viwanja vya ndege, bandari katika ziwa Tanganyika, upatikanaji wa umeme wa uhakika, pamoja na kuboresha huduma za jamii.
Kwa mujibu wa wa Mhandisi Manyanya alisema kutokana na mabadiliko hayo yaliyofanyika katika ukanda huo, ni fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuingia katika mikoa hiyo ili kuwekeza na hatimaye kuharakisha maendeleo ya wananchi.
“Wawekezaji wenye uzoefu wa biashara za hoteli za kitalii wanakaribishwa kujenga hoteli katika miji ya Kigoma, Mpanda, Sumbawanga, Mwambao mwa ziwa Tanganyika; pamoja na ujenzi wa mahoteli katika mbugas za hifadhi ya katavi, mahale na Gombe” alisema Manyanya.
No comments :
Post a Comment