Baadhi
ya wananchi na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni wakiwa katika mkutano
maalum ulioitishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
wa kukabidhiwa hati za umiliki wa mashamba ya kilimo katika maeneo yao.
Balozi
Seif Ali Iddi akimkabidhi Hati ya umiliki wa shamba Bibi Josephine
Yohana kwenye hafla maalum ya kumaliza mgogoro wa mashamba katika kijiji
hicho. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Balozi
Seif akimpatia Hati Bwana Mohd Ali Pili ya kumiliki eneo la kilimo
katika Kijiji cha Nguruweni ambako kuliibuka mgogoro uliosababishwa na
kuinbgizwa watu wasiohusika na maeneo hayo kwa kilimo.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
*****************************************************
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imewatahadharisha Wakulima wa Viijiji vya
Ndunduke, Nguruweni na Dole kuhakikisha kwamba maeneo ya kilimo
waliyokabidhiwa na Serikali kwa shughuli za Kilimo wanayatumia kama
yalivyopangwa na kukubalika na pande hizo mbili.
Wakulima
hao wakaonywa kuwa ye yote atakaeamua maeneo hayo kuyakata viwanja kwa
ajili ya kujenga nyumba au kuyauza kwa mtu mwengine aelewe kwamba
Serikali italazimika kumnyang’anya mkulima huyo mara moja.
Kauli
hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi wakati akikabidhi hati za umiliki wa mashamba ya kilimo kwa ajili
ya wakulima 40 kati ya 181 wa Kijiji cha Nguruweni waliokuwa
wakiilalamikia Serikali kwa kipindi kirefu kuidhinishiwa mashamba
wanayoyatumia ili kuendeleza shughuli zao za Kilimo.
Balozi
Seif alisema wapo baadhi ya watu wenye tabia ya kuomba mashamba au eka
kwa kisingizio cha kuendeleza kilimo lakini badala yake hujenga tamaa
inayowaelekeza kuanza kukata viwanja na kuuzia watu wengine.
“
Nataka nitahadharishe kabisa kwamba Mkulima ye yote atakayediriki
kutumia fursa aliyopewa na Serikali ya kuendeleza kilimo kwenye shamba
alilokabidhiwa na akaamua kufanya vyengine afahamu kwamba Serikali
haitasita kunyang’anya shamba hilo mara moja “. Alitahadharisha Balozi
Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwapongeza wakulima hao wa
Nguruweni kwa ustahamilivu wao mkubwa waliouchukuwa kwa kipindi kirefu
kufuatia mgogoro wa maeneo waliyokuwa wakitumia kwa shughuli za kilimo
baadhi yake kupewa watu wengine.
Balozi
Seif alisema ustahamilivu huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kuendeleza
amani na utulivu kwenye Vijijini hivyo vya Nguruweni, Ndunduke pamoja
na Dole ambayo imeleta faraja kwa Serikali Kuu kwa vile haikuathiri
shughuli za kila siku za kijamii.
Aliwakumbusha
wakulima hao kwamba hivi sasa ni muda muwafaka wa kuendeleza shughuli
zao za kilimo kwa vile wameshakuwa na uhalali wa kufanya hivyo katika
maeneo waliyopewa na Serikali.
Alifahamisha
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikisisitiza na
kuhimiza kilimo kwa vile sekta hiyo bado inaendelea kuwa muhimili Mkuu
wa uchumi wa Taifa hili.
“
Serikali imekuwa ikihimiza na kusisitiza umuhimu wa kilimo. Lakini
Mkulima hawezi kuendeleza kilimo bila ya kuwa eneo la kilimo, sasa kwenu
nyinyi hili suala linaonekana kuondoka “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati Maalum
aliyoiunda kushughulikia mgogoro huo wa mashamba ambae pia ni Mkuu wa
Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi kwa kushirikiana vyema na
watendaji wa Wizara za Kilimo na Ardhi na kuutatua mgogoro huo wa muda
mrefu.
Mapema
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Ali Juma alisema
Taasisi za Kilimo na Ardhi zililazimika kufanya uhakiki wa kina ili
kuwatambua wakulima halali waliokuwa wakistahiki kupatiwa hati hizo.
Nd.
Ali alisema uhakiki huo ulioshirikisha pia Masheha wa Vijiji
vilivyohusika na mgogoro huo vya Nguruweni Ndunduke na Dole umeibua
wakulima wapatao 181 ambapo wakulima 40 kati ya hao wamethibitika
kupatiwa hati hizo kwa awamu ya kwanza.
Naibu
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili alieleza kwamba kazi
ya uhakiki sambamba na uchambuzi kwa wakulima wa Kijiji cha Dole
imeshaanza rasmi na inatarajiwa kukamilika katika kipindi kifupi
kijacho.
Akitoa
shukrani zake Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyounda na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozib Seif kushughulikia mgogoro huo wa mashamba
ya vijiji vya Nguruweni, Ndunduke na Dole Mh. Abdulla Mwinyi alisema
Wakulima wa Vijiji hivyo wanapaswa kupongezwa kwa umahiri wao wa
ustahamilivu kufuatia mgogoro huo wa mashamba kwenye eneo hilo.
Hata
hivyo Mh. Abdulla Mwinyi ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi
amewaomba wale wakulima ambao bado mgogoro wao haujapatiwa ufumbuzi
waendelee kuwa na subra kwa vile Serikali kupitia Uongozi wa Kamati hiyo
unajitahidi katika kukamilisha mchakato huo.
Akitoa
shukrani kwa Niaba ya Wakulima hao Mmoja wa Wazee wa Vijiji hivyo Mzee
Kitwana Mustafa alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi kwa ujasiri na uungwana wake aliouchukuwa wa kutimiza
ahadi aliyowapa mwaka jana wa kumalizika kwa kadia hiyo.
Mzee
Kitwana alisema wakulima wa Vijiji hivyo wamefarajika na hatua
iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwatatulia
kero lililokuwa likiwasumbua kwa miaka mingi iliyopita.
“
Ile furaha yetu tuliyonayo leo kama tumengeruhusiwa basi tunatamani
tukubebe na matope yetu Mzee wetu kwa jinsi ulivyotujali na kututhamini
kwa katambua kwamba tulikuwa tukisumbuka kweli kweli “ Alionyesha
furaha yake Mzee Kitwana.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwahi kutoa ahadi
kwa wakulima hao wa Nguruweni, Ndunduke na Dole kwamba Serikali
itayagawa maeneo yote ambayo kamati aliyoiunda tarehe 14 Disemba Mwaka
2012 Chini ya Mwenyekiti wake Mh. Abdulla Mwinyi kufanya uhakiki wa
mashamba yote yaliyoleta mgogoro.
Wakulima
hao waliwahi kutoa shutuma kali kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif dhidi ya watendaji na Maafisa wanaosimamia Ardhi, Kilimo
wakiwemo pia Viongozi wa ngazi ya kati wa Serikali kwa vitendo vyao vya
kuingiza wakulima waliokuwa hawahusiki na mashamba hayo.
Watendaji
hao walituhumiwa na wakulima hao kuvuruga jukumu walilopewa la
kusimamia maandalizi ya utolewaji wa nyaraka kwa wakulima 28 wa awamu ya
kwanza waliokubalika kupatiwa hati za umiliki huo chini ya aliyekuwa
waziri Kiongozi wa mwisho wa SMZ Mh. Shamsi Vuai Nahodha.
Serikali
ililazimika kuzuia utolewaji wa hati hizo kufuatia hitilafu
zilizojichomoza za kupandikizwa baadhi ya watu wasiohusika jambo ambalo
lilisababisha mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima hao na watendaji
waliopewa jukumu la kusimamia suala hilo.
No comments :
Post a Comment