Na HERIETH MAKWETTA
'UGUMU
wa Maisha ni Kipimo cha Akili'. Huu ni usemi uliozoeleka katika maisha
ya kijamii hasa kwenye miaka ya sasa ambapo hali ya uchumi imekuwa
ikizidi kuwa ngumu.
Katika
ugumu wa maisha huo kuna walioshindwa kabisa kujikwamua hadi kukata
tamaa. Lakini kuna ambao wameutumia ugumu huo kutafuta namna ya
kujikomboa, ndiyo wanaozungumzia kwenye usemi huu.
Mmoja
wa watu hao ni mtangazaji ambaye pia ni Mmiliki wa Local Media
Entertainment, kampuni inayoendesha vipindi vya televisheni vya
'Wanawake Live' na 'Bongo Movie', vinavyorushwa na Kituo cha EATV,
mwanadada Joyce Kiria.
Utumwa
pasipo malipo sahihi na kutokuwa na uhuru wa maamuzi, vilikuwa sehemu
ya maisha yake kwa muda mrefu. Ilikuwa ni baada ya kumaliza elimu yake
ya msingi.
"Unajua
natoka katika familia ya hali ya chini, hivyo nilipomaliza Darasa la
Saba sikuwa na namna ya kuendelea na masomo," anasema.
"Nilianza kwa kufanya kazi za ndani za u-hausigeli, nilifanya kazi hii kwa miaka miwili. Sikuifurahia sana.
"Baadaye
niliona nisonge mbele, niliiacha kazi hiyo na nikajiunga katika genge
la mama ntilie, nilifanya kazi hapo kwa muda mpaka nilipoamua kuanza
kuchoma chapati."
Hata
hivyo anasema hakudumu na kazi hiyo kwani hakuwa akipatana na moto
hivyo akatafuta kazi katika kiwanda cha mablanketi, Chang'ombe jijini
Dar es Salaam.
"Nikafanya
kazi kwa muda pale lakini baadaye nikapata nafasi ya kazi katika duka
moja Kariakoo, jijini Dar es Salaam, hapo ilikuwa tayari imefikia mwaka
2000," anaongeza.
"Niliendelea na kazi yangu na baadaye nilipata mtaji wa kuniwezesha kufungua biashara yangu."
Anasema
alianza biashara zake rasmi kwa kupigisha simu katika vibanda vidogo,
mtaji ulikua na baadaye alifungua duka la vifaa vya shule na mapambo,
lakini baadaye akairudia biashara ya nguo.
"Baada
ya kufanikiwa kukuza mtaji wangu, niliingia tena katika biashara ya
nguo, na nikaanza kununua nguo za jumla kutoka Dubai, Falme za Kiarabu,"
anasema.
"Siku
moja nikaenda na kununua nguo mwenyewe huko Falme za Kiarabu. Nilirudi
na kuona nguo hizo zimejaa sana Kariakoo na bei yake ipo chini, hapo
ndipo mtaji wangu ukafa au kwa maneno mengine nifilisika."
Anasema
baada ya kushindwa biashara akaamua kumwona, Amina Chifupa (sasa
marehemu) ambaye alikuwa mteja wake wa nguo na kumweleza shida yake.
"Amina
ambaye wakati huo alikuwa anafanya kazi redio ya Clouds akanishauri
nianze utangazaji kwani aliona nina kipaji, hivyo nilianza kazi hiyo
pale Clouds mwaka 2006. Mwaka 2008 nikaolewa," anasema.
KUVUNJIKA KWA NDOA YA AWALI
Joyce, ambaye sasa ni mke halali wa Henry Kilewo, ndoa yake ya kwanza ilikuwa mwaka 2008 alipooana na Nelson Joshua 'DJ Nelly'.
"Muda
mfupi baada ya ndoa nikaanza kuonja machungu yake, niliishi maisha
ambayo sikuchagua, hii ilikuwa ni baada ya kuolewa," anasema.
"Niliamua
kuachana na mume, unajua ilifikia hatua nilihisi ningeweza hata
kuwekewa sumu katika chakula, yalikuwa ni maisha ya chuki.
"Hapo
ndipo ukawa mwanzo wa kuyajua mengi ambayo niliamua rasmi kuanza
kuyafanyia kazi nikiwa kama mwanamke niliyejitolea kutetea haki za
wanawake."
Anasema alianza kwa kudai talaka ambayo ilikuwa ngumu kutolewa kwani ndoa aliyofunga ilikuwa ni ya Kikristo.
"Nilifanikiwa
kupewa talaka yangu na hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuanzisha kipindi cha
Wanawake Live nikiwa na dhamira ya kweli ya kutetea Haki za Wanawake.
WITO WAKE KWA JAMII
Joyce ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro, anasema tatizo lililopo hapa nchini ni mfumo dume, ambao umekithiri.
"Mwanaume
anasahau kutunza familia yake na kutokomea kusikojulikana, kwa sababu
ya uchumi mdogo familia yake inaingia kwenye taabu, hali hii haivumiliki
na ndiyo mwanzo wa kuvunjika kwa ndoa nyingi," anasema.
"Pia
changamoto za kimaisha ni nyingi, wapo wanawake wenye kipato, lakini
kutokana na mfumo dume wanalazimika kuacha kila kitu kikiwa chini ya
waume zao ambao baadaye huwasaliti."
Anasema
kupitia kazi yake ya sasa amepania kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ili
iachane na na mfumo huo kuweza kutoa haki sawa kwa wote.
Habari hii kwa hisani ya gazeti la Mwanaspot.