Na Ali Mohammed, Coconut Fm, Zanzibar.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Maalim Seif Sharif Hamad, ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuandaa utaratibu wa kutoa elimu ya Hijja kwa Waislamu ili kuwahamisha kutekeleza Ibada hiyo wakati unapofika.
Amesema waislamu wengi wanao uwezo wa kwenda Hijja lakini bado hawajapata taaluma ya kutosha juu ya namna ya kutumia uwezo walionao kutekeleza ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano ya Kiislamu.
Al-haj Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo katika msikiti mkuu wa muembeshauri mjini Zanzibar alipokuwa akiwaaga rasmi waislamu wanaotarajia kwenda Makka kutekeleza ibada ya hijja kuanzia kesho.
Amesema Serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa mahujaji wanaondokana na usumbufu katika kipindi chote cha safari yao, na kuzitaka taasisi zinasafirisha mahujaji kushirikiana ili kuwaondoshea usumbufu mahujaji.
Aidha amesema Serikali itaendeleza utamaduni wa kuwaaga rasmi mahujaji kila wanapoondoka kwa vile hili ni miongoni mwa masuala muhimu katika nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Al-Hajj Aboubakar Khamis Bakar amezipongeza taasisi za Hijja Zanzibar kwa kuunda Umoja ambao utasaidia kuboresha safari za Hijja na kuzifanya kuwa nyepesi.
Ameziomba taasisi hizo kushikamana na kuendeleza umoja, bila ya kujali biashara ambayo mara nyingi husababisha kuleta tofauti katika taasisi kama hizo.
Nae Katibu wa Umoja wa taasisi za Hijja Zanzibar (UTAHIZA) Sheikh Hassan Rashid Mohd amesema licha ya gharama za Hijja kuongezeka, lakini idadi ya mahujaji imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka hapa Zanzibar.
Amewaomba waislamu wenye uwezo kufanya haraka kuitekeleza Ibada hiyo na kuwasaidia wengine kufanya hivyo, ili kuwafanya waislamu wengi zaidi za Zanzibar kutekeleza Ibada hiyo.
No comments :
Post a Comment