Misri na Cameroon zina kibarua licha ya ushindi wa Kombe la Mataifa mara kumi na moja baina yao. Timu hizi zina shughuli pevu kuvuka michuano ya kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.
Misri iliyo katika chungu chenye moto inahitaji ushindi dhidi ya Bafana bafana mjini Cairo siku ya jumapili vinginevyo itaondolewa kwenye mashindano iliyoyatawala na kushinda mara saba ikiwa ni mara tatu mfululizo hadi sasa.
Endapo Cameroon itashindwa ugenini Senegal siku ya jumamosi huenda tukawakosa wachezaji kama Samuel Eto'o wa Inter Milan na Alex Song wa Arsenal.
Michael Essien anatarajiwa kurejea uwanjani kwa mara ya kwanza kuinua matumaini ya Ghana baada ya kukaa nje ya mechi za kimataifa kwa zaidi ya mwaka mzima Black stars itakapochuana na Jamhuri ya Congo.
Timu zitakazomaliza kwa pointi bora katika nafasi ya pili zitafuzu timu 12 zilizofuzu moja kwa moja kujiunga na mwenyeji wa mashindano haya Gabon na Equatorial Guinea. Hata hivyo Misri na Cameroon hazijaonyesha kiwango cha hata kufuzu kupitia mlango wa nyuma.
Timu hizi zinakabiliana na timu zilizowararua dakika ya mwisho wakati wa michuano ya awali.
Misri inaburura mkia wa kundi G na itakosa kufuzu tangu mwaka kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1978 endapo watachapwa na Bafana Bafana na kisha Niger iliyo katika nafasi ya pili ishinde mechi yake dhidi ya Sierra Leone.
Tayari mechi hiyo iliyopigiwa debe vilivyo imehamishiwa uwanja wa kijeshi badala ya uwanja mkubwa wa Kimataifa kwa hofu ya mashabiki wake kuzusha ghasia endapo matokeo yatakwenda kinyume na matarajio yao.
Cameroon ilipoteza mecji yake dhidi ya viongozi wa kundi E Senegal ambapo Simba hao wa nyika wanajikuta mkiani mwa kundi hilo kwa pointi tano.
Ikumbukwe kuwa Cameroon ilishinda Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2000 na 2002 na haijawahi kukosa kushiriki fainali ya Kombe hili kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Mcheza kiungo wa Chelsea Michael Essien alifanya mazowezi na Timu yake ya Taifa wiki hii na anaonekana kuwa tayari kushiriki mechi ya ijumaa.
Ghana inasimama kileleni sawa na Sudan kwa pointi saba katika kundi 1 na haiwezi kuruhusu kupoteza dhidi ya Congo huku Sudan ikichuana na Swaziland ambayo haijashinda mechi hata moja.
Wakati huo huo Nigeria inatazamia kuendelea na hatua yake ya maendeleo chini ya Kocha mpya Samson Sia sia watakapoitembelea Ethiopia. Nigeria iko nyuma ya Guinea kwa tofauti ya pointi. Ivory Coast ikishinda kwa mara ya nne itafuzu kutoka kundi H iwapo Rwanda itashindwa kuiangusha Burundi.
Botswana ambayo haikutarajiwa itajisafishia mambo ikiwa itainyoosha Malawi katika kundi K.
Ni katika kundi hili ambapo bingwa wa mwaka 2004 Tunisia inakabiliwa na aibu ya kushindwa kufuzu ikiwa iko nyuma ya Botswana na Malawi ikitazamia mchuano dhidi ya Chad.Ni timu mbili pekee zitakazofuzu kutoka kundi K.
Libya pamoja na matatizo yake inaongoza kundi C kwa pointi moja mbele ya Zambia ikielekea Gabon na Equatorial Guinea mwezi Januari.
No comments :
Post a Comment