Na Josephat Lukaza wa Proin Promotions Limited - Dodoma
Hii ni
baada ya washindi watatu kutoka Kanda ya Kati kupatikana katika
shindano la kusaka vipaji vya kuigiza lililoendeshwa na Kampuni ya Proin
Promotion Limited (PPL). Fainali ya kuvisaka vipaji kwa kanda ya Kati
ilifanyika jana Mnamo tarehe 15 April 2014 Mkoani Dodoma na washindi
kutangazwa na Jaji Mkuu wa shindano hilo, Roy Sarungi aliyesaidiwa na
Yvonne Chery ‘Monalisa’ na Single Mtambalike ‘Richie Richie.’
Roy
kwa kusaidiana na Yvonne Chery ‘Monalisa’ na Single Mtambalike ‘Richie
Richie.’ aliwatangaza Joyce Rebeca, Moses Obunde na Mwinshehe Mohamed
kuwa washindi wa shindano la kusaka vipaji vya kuigiza Tanzania
lijulikanalo kama Tanzania Movie Talents ambapo kila mmoja alipewa
zawadi nono ya Sh 500,000. Shindano hilo liliwashirikisha washiriki 500,
lakini ni washiriki watano wenye vipaji waliofanikiwa kuingia tano bora
na baadaye majaji walifanya kazi kubwa ya kuwachagua na kuwatangaza
washindi watatu.
Mshiriki
mkubwa kuliko wote , Idrisa Ally (40), alionesha kipaji cha hali ya
juu cha kuigiza na alizawadiwa na majaji Sh 100,000. Idrisa hatakwenda
kushiriki fainali za mashindano hayo zinazotarajiwa kufanyika
Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam kutokana na umri wake kuwa mkubwa
kuliko kigezo cha umri kilichowekwa cha kuanzia miaka 14 hadi 35, ingawa
majaji waliahidi kuwasiliana naye kwa lengo la kuendeleza kipaji chake
umri wake utakaporuhusu.
“Tumebaini
kuwa Kanda ya Kati hususani Mkoa wa Dodoma kuna vipaji vingi vya sanaa
ya uigizaji na katika hili Idrisa Ally ametuthibitishia yeye ni mzee
mwenye kipaji, lakini amedhihirisha kuwa ana kipaji cha kuigiza,”
anasema Jaji Mkuu wa shindano hilo, Sarungi anasema sanaa ya uigizaji ni
muhimu kwa vijana, kwa vile sasa hutoa fursa ya ajira ambapo
imewawezesha vijana wengi nchini kujiajiri wenyewe na kuimarika
kiuchumi.
“Ni
matumaini yangu kuwa kwa washindi hawa wa Kanda ya kati hawataishia hapa
watajiendeleza zaidi kwani uigizaji sasa ni ajira,” anasema.
Mshiriki Moses Obunde alishindwa kuzuia furaha yake baada ya kutangazwa
mshindi, aliangua kilio kuashiria furaha aliyokuwa nayo na kuufanya
ukumbi mzima kutaharuki.
Ofisa
Uhusiano wa Proin Promotion Limited (PPL), Josephat Lukaza, ambao ndio
waratibu na waandaaji wa shindano hilo la kusaka vipaji vya uigizaji,
anasema mashindano hayo yanaendeshwa kikanda, ambapo kwa kuanzia
walianza kusaka vipaji kwa Kanda ya Ziwa na Kumalizika Jana katika Kanda
ya kati Mkoa wa Dodoma na hatimaye zoezi hili kuamia Kanda ya Juu
Kusini ambapo usaili utafanyika Mkoani Mbeya kuanzia tarehe 19 April.
“Baadaye
tutaelekea Kanda ya Njanda za Juu Kusini lakini tunashukuru kwa
ushirikiano tulioupata kwa wakazi wa Kanda ya Kati, tumepata washiriki
600, ambao tuliwachuja hadi kuwapata washindi watatu waliokidhi vigezo
tulivyovihitaji,” anasema Lukaza. Baadhi ya vigezo kwa mujibu wa Lukaza,
vilikuwa ni mshiriki kuwa na umri kuanzia miaka 14 hadi 35,
anayejiamini, mbunifu, anayemiliki jukwaa na igizo lake libebe ujumbe wa
kuelimisha.
Anasema
lengo la PPL kuzungukia kanda hizo sita nchini ni kuhakikisha kuwa
inavisaka vipaji vya vijana kupitia sanaa ya maigizo, ambavyo
vimejificha ili viendelezwe na kampuni yake. “Tumeamua kuwekeza katika
sanaa maana sanaa ni fursa kama zilivyo fursa zingine nchini na ni
matumaini yetu kuwa jamii itatuunga mkono katika safari ndefu tuliyo
nayo ya kuvisaka na kuviendeleza vipaji,” anaeleza ofisa huyo uhusiano.
Anasema PPL inaendesha shindano hilo kwa kanda sita nchini ambazo ni Kanda ya Ziwa, Magharibi, Pwani, Kati, Kaskazini na Kusini.
“Kwa
sasa tumeanza na mikoa sita, lakini matarajio yetu ya baadaye ni
kuifikia mikoa yote nchini ambapo tunaamini kuna vipaji vingi vya
wasanii vimejificha ili waweze kupata ajira kupitia vipaji vyao,”
anasema na kuongeza kuwa mshindi wa jumla baada ya mashindano ya kikanda
kumalizika atapatikana Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambako
ataondoka na zawadi nono ya Sh milioni 50.
Anasema
usakaji vipaji hivyo huendeshwa kwa umakini na umahiri mkubwa kupitia
kwa majaji na watu wenye utalaamu wa tasnia ya filamu na teknolojia ya
habari (IT) walio chini ya kampuni yake, ambao pia huzingatia miiko na
maadili ya kazi hiyo kwa kila mshiriki. Anasema PPL imesajiliwa rasmi
mwaka 2013 kupitia Sheria ya Usajili wa Makampuni ambayo hushughulika na
ukuzaji wa sanaa ya filamu nchini.
“Pia
tunashughulika na usimamizi wa uzalishaji wa filamu nchini, uzalishaji
na usambazaji wa DVD na filamu zilizokamilika kuingia sokoni na
matarajio yetu ya baadaye ni kuwa kampuni bora katika Bara la Afrika,”
anaeleza. Wakizungumza na gazeti hili, washindi waliobuka kidedea
waliwashukuru waandaaji wa shindano hilo kwa kuibua vipaji vyao ambavyo
wanasema visingeweza kutambulika.
Crecensiah
anasema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwibua katika shindano hilo na
kumwezesha kuwa mshindi, ambapo sasa anaamini kuwa ndoto yake ya kuwa
msanii wa kimataifa imetimia. “Namshukuru
Mungu kwa yote, lakini zaidi niwashukuru waandaaji wa shindano hili kwa
kutumia muda wao na fedha kuvisaka vipaji, binafsi naona kiu yangu ya
kuwa muigizaji wa kimataifa imetimia, nitaongeza juhudi kubwa katika
tasnia ya filamu,” anasema msanii huyo. Naye Janeth anasema penye nia
pana njia, kwa madai kuwa alikuwa na kiu ya kuwa msanii wa kuigiza kwa
muda mrefu hasa baada ya kuwaona wasanii mbalimbali kupitia luninga
nchini.
“Kwa
kweli naweza kusema nimepata maji ya kunywa dhidi ya kiu yangu ya kuwa
msanii, ni kazi ambayo nilikuwa naipenda tangu nikiwa mtoto namshukuru
sana Mungu na waandaaji wa shindano hili la kusaka vipaji vya kuigiza,”
anaeleza mshindi huyo. Kwa upande wake, Joshua Wambura anasema ushindi
wake ni mwanzo wa safari yake ndefu katika kuingia katika tasnia ya
filamu ndani na nje ya nchi.
No comments :
Post a Comment