Baada ya mafanikio makubwa ya Dow Live Earth Run for Water 2010- sehemu ya mradi wa kimataifa wa kutatua tatizo la janga la ukosefu wa maji ulimwenguni kote, kampuni ya simu za mkononi tiGo Tanzania pamoja na Spearhead Africa Limited inaamini kwamba mwamko huu upewe kipaumbele kwa kuzingatia kwamba janga hili la ukosefu wa maji bado halijatokomezwa. Huu ni mwaka wa pili kwa shughuli hii ya uchangajishaji fedha kuendeshwa nchini na kampuni ya Spearhead.
Lengo la shughuli hii kwa mwaka huu ni kuchimba visima vyenye urefu wa mita 200 na 100 ili kutoa ufumbuzi kwa zaidi ya wakazi 100,000 waishio Bagamoyo ambao hawana uwezo wa kupata maji safi na salama.
Mwaka huu kampuni ya simu za mkononi ya tiGo imejitolea kusimamia shughuli nzima ya Walk for Water na kampuni ya Spearhead na imefurahia mchango huo wenye lengo la kutokomeza janga hili. tiGo Tanzania kama moja ya wadhamini wa Dow Live Earth Run for Water 2010, pamoja na kuona mwamko wa wananchi kujitokeza kwa wingi kutokomeza janga hili, tiGo wameamua kutoa msaada huu kama sehemu ya huduma zao kwa jamii ambayo imewazunguka.
Malengo ya matembezi haya ya hisani ni:
1. Kutaarifu umma na wadau wa maji kuhusu janga la maji na ufumbuzi wa janga hili.
2. Kutoa fursa kwa wadau wote wa maji kutoa elimu ya kutunza maji ,matumizi mazuri ya maji na kutoa taarifa kuwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kusaidia kutatua janga hili.
3. Kuhamasisha mashirika kushiriki kwenye mbio/matembezi ya hisani, kuonesha bidhaa au huduma zao na kutoa mchango kwa mradi teule wa naji.
4. Kuchangisha fedha kwa ajili ya mradi endelevu wa maji utakaotoa huduma kwa jamii kwa muda mrefu.
Afisa uhusiano wa Tigo Tanzania, Mr. Jackson Mmbando alisema,” Tunafuraha kuwaletea shughuli hii ya kuchangia mradi wa maji na tunawahamasisha waandaaji wengine kuwa na moyo kama huu. Pia hii sio changamoto tu kwa Bagamoyo bali kwa maeneo yote ya Tanzania. Tunawahimiza wachangiaji na watu binafsi kujisajili na kuchangia mradi huu.”
“Kupitia Tigo Walk for Water, tunatarajia kupata fedha taslim shiligi Milioni 60 za Tanzania kwa ajili ya mradi huu, kwa msaada wa Ifakara Health Institute, tumeweza kutambua maeneo ya kuyapa kipaumbele ya kuchimbwa visima vyenye urefu wa mita 200 na 100 ili kuipatia jamii maji salama katika kata za Bagamoyo.”
tiGo Walk for Water itafanyika kwenye uwanja wa maegesho ya magari ya Mlimani City Mall siku ya jumamosi, 16 Aprili 2011. “Tunawashukuru Tigo kwa kutuletea shughuli hii ya kuchanga fedha. Tunategemea wale wote walioshiriki mwaka jana kwenye uwanja wa taifa watatuunga mkono kwa kujisajili kwa matembezi au mbio za kilometa 6, umbali ambao unakadiriwa ni wastani wa umbali wanaotembea wanawake wengi na watoto kila siku kutafuta maji safi ya kunywa.” alisema Bertha Ikua- Meneja Huduma kwa wateja wa Kampuni ya Spearhead Africa.
Mradi wa maji wa Bagamoyo iliyopo chini ya Ifakara Health Institute ndio utakaonufaika na Tigo Walk for Water 2011.
Bertha Ikua aliongezea “Kuna vijiji vingi Bagamoyo ambavyo wananchi wake hawawezi kupata maji safi na salama.Visima vingi ni vifupi na vinakauka wakati wa kiangazi, mito siyo salama na ipo mbali na makazi ya watu, maji ya mvua ni ya msimu na maji ya bomba ni kwa ajili ya watu wachache wenye uwezo wa kulipa bili ya kila mwezi.
Baadhi ya maeneo ambapo kina cha maji ni kirefu, mara nyingi ni rahisi kuchimba visima venye sifa ya ubora kwa gharama nafuu lakini maeneo ambayo kina cha maji ni kifupi tutahitaji kuchimba vissima venye vina virefu zaidi ya mita 100 ili kupata maji.”
Usajili wa mtu binafsi kwa ajili ya matembezi ya maji ni shilingi 3000 na usajili huo utaanza tarehe 28 Machi katika Makao Makuu ya Tigo yaliyopo barabara ya Nyerere na mtaa wa Ohio, Shoppers Plaza Masaki na Mikocheni, City Supermarket iliyopo Harbour view, Shoprite ya barabara ya Pugu, Village Supermarket iliyopo Sea Cliff Village, Novel Idea yiliyopo mtaa wa Ohio, maduka na ofisi zote za hoteli ya Oysterbay pamoja na Mlimani City Mall.
Kampuni mbalimbali, Balozi, mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali yanahamasishwa kushiriki siku hii kwa kuifanya iwe siku ya pamoja ya wafanyakazi na kujisajili kutembea kwa pamoja kama kampuni au shirika kupitia anuani ya barua pepe kahenga@spearheadafrica.com au kwa kupiga simu 0713 252 254.
No comments :
Post a Comment