Abeti Masikini "The Nightengale of Zaire" alipokuwa akitamba enzi zake
*Mkali wa kike wa muziki kizazi kipya anayetisha sasa
*Ni baada ya akina mama kushindwa 'kuzalisha' vipaji
*JB Mpiana 'alizima' zake, amkubali kwa asilimia zote
katika safu hii ya wanamuziki na muziki wa Afrika, hasa wa nchini Kongo ambao kwa kiasi kikubwa umeteka soko la muziki karibu Afrika yote, nitazungumzia sauti za gharama za akina mama.
Nimekuwa nikijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu ni kwanini wanamuziki wa kike, nyota waliowahi kuwika miaka ya nyuma nchini Kongo kutoka enzi ya akina Abeti Masikini hadi leo washindwe kuwarithisha kipaji hicho kwa mabinti wa kizazi cha sasa?
Hii imekuwa ni tofauti kubwa kwa upande wa wanaume, ukizungumzia kutoka enzi ya akina Dkt. Nico Kasanda, Luambo Rwanzo Franco Makiadi, uje enzi za akina Papa Wemba, Bozi Boziana, Aurus Mabele, Koffi Olomide, 'ushuke' kwa akina JB Mpiana, Werrason Makanda, Alain Mpela, na sasa wanaotamba katika kizazi kipya akina Ferre Gola 'Shetani' na Fally Ipupa.
Hao niliowataja wote nitawaelezea katika makala yatakayofuata baada ya haya, katika kuwachambua wanamuziki wa kiume wa Kongo, wakali na wenye sauti za gharama, kuanzia ya kwanza kama ya Mandal Chante, Lora Mwana Dindo na Papa Wemba hadi nzito za akina Madilu System, sasa nirudi kwa malkia hao wa Kongo.
Ni ukweli usiopingika kwamba wanamuziki wa kiume wamekuwa wakirithishana ama iwe rasmi, mfano kutoka kwa mzazi hadi mtoto kama ilivyo kwa Dindo Yogo aliyerithiwa na mtoto wake Lora Dindo Yogo, Vick Longomba aliyerithiwa na Lovy Longomba na Awilo Longomba, au urithi usio rasmi kwa maana ya kizazi cha wanamuziki kujizalisha chenyewe kihistoria.
Kama nilivyoeleza tumeshuhudia makundi mengi yakichuana na kuleta ushindani mkubwa wa muziki tangu enzi za akina Dkt. Nico hadi leo hii tunaendelea kushuhudia akina Fally Ipupa wanavyochuana na Ferre Gola na wengine wengi.
Hali hii iko tofauti kwa wanawake, ushindani uliokuwepo enzi ya akina Abeti Maskini, enzi ya akina Mbilia Bel alivyokuwa akilumbana na wifi yake M'Pongo Love na baadaye Faya Tess, leo hii hakuna.
Meje 'MJ 30' aliyejitiwisha mikoba ya T Shala Mwana akimwaga radhi kwa kunengua bila nguo ya ndani (sehemu iliyozzibwa) ndiye anayekuja juu kwa sasa nchini Kongo.
Hakuna kizazi cha wanamuziki wa kike cha kujisifia tangu hao akina Mbila Bel na Tshala Mwana walipowika na kuondoka zao katika ushindani na sasa wakipiga muziki wa 'vilabuni' tu hata kama wanatoa albamu, lakini muziki wao si wa ushindani na wanaendelea kuwepo katika anga la muziki hata katika umri wao mkubwa ni kutokana na kukosa upinzani au ushindani wa kweli kwa wasanii wa kike wabichi.
Je, vipaji vyao hivyo vimerithiwa na akina nani? Hata kama si katika muziki wa dansi, tuzungumzie tu muziki wa kizazi kipya kama wa Zouk ambao kwa Wakongo (unapigwa na wanawake zaidi), nani anatisha? Ni wachache na zaidi nitakuelezea binti mmoja matata sana anayeibukia na kutisha katika fani hiyo kwa sasa.
Ni pengine ni kutokana na uhaba huo wa vipaji kwa upande wa watoto wa kike, na ndiyo maana wengi walikuwa wakifikiri kuwa, Monique Seka 'Queen of Afro-Zouk' ni raia wa Kongo, baada ya kutamba sana na albamu yake ya Missounwa.
Mwanamama huyu alitamba sana katika muziki wa Zouk, huyu ni mzaliwa wa Ivory Coast, alipoibukia katika anga la muziki, wengi walidhani ni 'toleo jipya' la muziki wa kizazi cha Kongo, lakini huyu ni raia wa Ivory Coast.
Ndiyo maana hapo juu nimeainisha kuwa akina mama hawa wa Kongo waneshindwa 'kuzalisha' kilicho bora kwa maana kushindwa kuibuka kwa mabinti wakali wa kizazi kipya katika muziki wa Kongo, lakini pia nikasema kuwa, hata kwa muziki wa kizazi kipya imekuwa tabu, kwa maana ni mwanamke gani kwa sasa nchini Kongo anayetamba kama ilivyo kwa akina Fally Ipupa, au kama ilivyokuwa enzi za akina M'Pongo Love?
Kwa sasa huyo anayetisha anajulikana zaidi kwa jina la Meje Bula 30 pia MJ 30. Binti huyu ni mkali wa miondoko ya Zouk, anatisha kama alivyokuwa anatisha Tshala Mwana katika miondoko ya Mutuashi, lakini binti huyu naye amekuwa akimwaga radhi na zaidi ya Tshala Mwana, yeye anacheza bila nguo ya ndani na kumwaga radhi!
Nadhani kama ni kumrithi Tshala Mwana, huyu atakuwa zaidi ya urithi. Ukiachilia mbali na huyo, binti mwingine ambaye naweza kusema ni wa muziki wa kizazi kipya ni Tata Muasi, huyu anafanya muziki wa rhumba na ni mwanamuziki pekee wa kike wa Kongo anayefanyakazi zake Uingereza.
Tata Muasi amejijengea umaarufu nchini Uingereza kiasi cha kuitwa 'Queen of African rumba' au Malkia wa rhumba la Kiafrika na hasa, baada ya kuachia albamu yake katika CD na DVD Novemba 3, 2007 inayojulikana kwa jina la Mimitah.
Ukiondoa wasanii hawa mabinti wawili wanaotesa kwa sasa, ambapo nitawazungumzia baadaye katika makala haya, zaidi ya hao hakuna, na labda tuangalie malkia wa Kongo katika uimbaji na hata unenguaji waliotamba tangu miaka ya 1960, wakati wa akina malakia Abeti Masikini.
*Abeti Masikini
Mkali huyu alizaliwa mwaka 1956, huko Kisangani, Congo (DRC). Kwa miaka 9 ya kwanza katika maisha yake, baba yake alikuwa akimfundisha kupiga kinanda (organ).
Kisha baadaye akaanza kuimba kwaya ya Kanisa la Kilomoto na katika matamasha yaliyohusisha familia. Uimbaji wake ulikuja baada ya yeye kuvutiwa na mwimbaji mmoja wa Kifaransa aliyeitwa Edith Piaf.
Malkia wa miondoko ya Mutuashi, Tshala Mwana, picha ya kushoto alivyokuwa akitamba enzi za ujana wake na picha ya kulia ni ya juzi alivyotumbuiza hapa nchi Tanzania, Desemba mwaka huu alipokuja na JB Mpiana.
Juhudi zake Abeti, zilimfanya aweze kushinda mashindano ya vipaji ya kuimba yaliyoandaliwa na Piaf. Wengine waliomvutia hadi kujikita zaidi katika muziki ni wanamuziki wa kike Miriam Makeba wa Afrika Kusini na Mireille Matheiu wa Ufaransa.
Ushindi alioupata katika mashindano ya vipaji ya uimbaji yalimfanya Abeti ajulikane sana jijini Kinshasa na muda mfupi akapachikwa jina la kisanii na kuanza kuitwa "the Nightengale of Zaire".
Mwaka 1971, alikutana na mtengeneza muziki (prodyuza) raia wa Togo aliyeitwa Gerard Akueson. Akueson alikuwa akifanya kazi na msanii Bella Bellow, mwanamuziki wa Togo, ambaye ndiye aliyekuwa anamrekodia kazi katika studio yake.
Baada ya kukutana na prodyuza huyo, akajikuta akiimarika zaidi katika muziki wa Kiafrika hasa katika miondoko ya 'soukous parfume' na baadaye rhumba.
Mwaka 1972 alialikwa na Bruno Coquatrix, kufanya onesho katika ukumbi wa L'Olympia, Ufaransa na mambo aliyofanya katika onesho hilo yalikuwa ni makubwa na kuwa chanzo cha mafanikio yake katika muziki.
Katika onesho hilo la mafanikio, Abeti 'alikamua' ipasavyo mbele ya watazamaji wapatao 3,000, waliohudhuria na huo ukawa mwanzo wa mafanikio yake makubwa.
Mwaka 1974 akachaguliwa kuwa balozi wa Umoja wa Mataifa (UN), kutokana na kufanya vizuri katika albamu yake ya 'Bibile' kwa ushirikiano mkubwa na Gerald Akueson.
Maonesho mengine yaliyompatia heshima kubwa mwanamuziki huyu ambaye hapa Tanzania anafahamika zaidi kwa kibao chake cha 'Makayabu' ni aliyoyafanya China, hasa wakati wa mgomo wa Tien An Men Square mwaka 1989.
Hata hivyo maisha ya msanii huyu yalikomaa mwaka 1991, Abeti alifia jijini Paris, Ufaransa baada ya kuugua kwa muda mrefu na ilizuliwa kuwa msanii huyo alikufa kwa maradhi ya UKIMWI, japo hakuna taarifa zilizo rasmi kuhusu tetesi hizo.
Albamu yake ya Souvenirs Souvenirs ilitolewa miaka mitano, baada ya yeye kufariki, ilitolewa chini ya lebo ya Blue Silver katika CD mwaka 1996. Albamu zake nyingine ni Bibile ya mwaka 1975, 10e anniversair, 1er best of, En Colere, Je suis fache na Scandale de jalousie.
Kwa kifupi huyo ndiye Abeti Masikini, mmoja wa malkia wa Kongo aliyekuwa na kipaji au sauti ya gharama ambayo bado haijarithiwa na wasanii mabinti waliokuja au wanaoendelea kuja baada ya yeye kutoweka. Pengine katika muktadha huo, tumtupie jicho msanii, malkia mwingine wa Kongo aitwaye M'Pongo Love.
Je wanamuziki wa Tanzania tunajifunza nini hapa?
SOMA GAZETI LA MAJIRA KILA SIKU