Na Addolph Bruno
MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni ambaye pia ni mdau wa mchezo wa ngumi na mateke (Kickboxing) Iddi Azzan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika pambano la ngumi litakalowakutanisha mabondia Japheti Kaseba na Mada Maugo litakalofanyika Jumamosi ya tarehe 16 katika ukumbi wa PTA Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo lisilo la ubingwa linatarajiwa kuwa ni la uzani wa kati (middle) kilogramu 72 ambapo mshindi ataandaliwa kucheza na bondia Francis Cheka ambaye kwa sasa yupo katika maandalizi kucheza na Mmarekani John Upshaw hivi karibuni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Promota wa pambano hilo Siraji Kaike alisema maandalizi yanaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na mabondi wote kuwa katika afya njema wakiendelea na mazoezi.
Alisema awali Kamanda wa kanda maalumu Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni mlezi wa mchezo huo hapa nchini Suleiman Kova alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo lakini kutokana na kuzidiwa na kazi nafasi yake itachukuliwa na Azzan ambaye amethibitisha kushiriki.
"Tumefanya mazungumzo na mgeni rasmi yupo tayari kabisa kuja kusapoti na kila kitu kinakwenda swa wapenzi na wadau wote wakae sawa kutokana tumeyamaliza matatizo yote na matarajio ni kwamba huu ni miongoni mwa michezo mizuri iliyowahi kufanyika .," alisema promota huyo.
Alisisitiza kuhusu bondia Mada Maugo kugoma kutokana na kuzidiwa pointi mbili na mpinzani wake madai hayapo ambapo kamati ya maandalizi ilikaa nao na kukubaliana Kaseba afanye jitihada za kupunguza uzito jambo ambalo analitekeleza.
Kaike alisema kuhusu pambano la utangulizi ambalo awali lilitakiwa lifanyika kati ya Kamanda Kova na Iddi Azan imeshindikana kutokana na Kova kuzidiwa na kazi nyingi ambapo siku ya pambano atakuwa Jijini Arusha katika mkutano.
Alisema pambano hilo litatanguliwa na mengine mengi ya mabondia mchanganyiko wenye uzoefu na wanaoanza ili kuleta ladha kwa mashabiki wao watakaohudhuria ambapo yatakuwa ni ya uzito tofauti na mabondia wote watapima uzito na afya zao siku moja kabla ya mchezo huo.
No comments :
Post a Comment