Mwili wa mmoja kati ya waliopoteza maisha huko Loliondo.
Na Neville Meena na Mussa Juma, Samunge
IDADI ya watu waliopoteza maisha wakienda kupata tiba ya magonjwa sugu kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila katika Kijiji cha Samunge, Loliondo Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha imefikia 78.Habari ambazo Gazeti la Mwananchi limezipata na kuthibitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Dominick Lusasi zinasema idadi ya vifo hivyo ni ile iliyorekodiwa kuanzia Machi 11, mwaka huu.
IDADI ya watu waliopoteza maisha wakienda kupata tiba ya magonjwa sugu kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila katika Kijiji cha Samunge, Loliondo Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha imefikia 78.Habari ambazo Gazeti la Mwananchi limezipata na kuthibitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Dominick Lusasi zinasema idadi ya vifo hivyo ni ile iliyorekodiwa kuanzia Machi 11, mwaka huu.
"Kati ya Machi 11, mwaka huu tulipoanza kuchukua rekodi za waliokufa na Machi 29, watu 74 walikuwa wamethibitishwa kufariki dunia, lakini hivi karibuni nilipata taarifa kwamba watu wengine wanne wamefariki," alisema Lusasi.
Hata hivyo, idadi hiyo inaweza kuwa ndogo kuliko uhalisia kwani upo uwezekano mkubwa kwamba wapo waliofariki dunia na vifo vyao havikurekodiwa tangu watu walipoanza kufurika Samunge mwishoni wa Januari ,mwaka huu hadi Machi 11, 2011 utunzaji wa kumbukumbu ulipoanza.
Kwa mujibu wa uongozi wa Kijiji cha Samunge, watu 19 wamelazimika kuzikwa kijijini hapo kutokana na ama maiti kukosa ndugu au ndugu kutokuwa na uwezo wa kusafirisha maiti hivyo kuomba msaada wa Serikali.
Majina ya waliofariki Miongoni mwa waliopoteza maisha ni mke wa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mama Parceko Vincent Kone (55), watoto saba akiwamo mtoto wa miaka miwili, Bokye Mwilenyi Magoli, mkazi wa Kyang'ombe, Wilaya ya Rorya, mkoani Mara aliyefariki dunia Machi 25, 2011 sambamba na wagonjwa wengine 10 waliofariki dunia siku hiyohiyo.
Taarifa ya Idara ya Afya ya Halmashauri ya Ngorongoro inawataja watoto wengine waliofariki dunia wakiwa Loliondo kuwa ni Fatma Hussein (5), mkazi wa Msambi - Kileche, Mwanga, Kilimanjaro; Athumani Omari (7), mkazi wa Ntiko, Singida; Tumaini Samson (10), mkazi wa Sengerema, Mwanza; Lesian Yuton (12) mkazi wa Dodoma Mjini na Jescar John (16) wa Dar es Salaam.
Mtoto mwingine aliyefariki dunia ni raia wa Kenya, Maximilian Shuku (12), mkazi wa Narok na raia mwingine wa nchi hiyo, Nori Makati (46) ambaye ni mkazi wa Usupuko.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, siku inayoongoza kwa vifo vingi ni Machi 24, 2011 ambayo watu 15 walipoteza maisha, ikifuatiwa na Machi 25 ambayo ilishuhudia wagonjwa kumi na moja wakifariki dunia hivyo kufanya jumla ya waliopoteza maisha kwa siku hizo mbili tu kufikia 26.
Majina ya watu wengine waliofariki dunia, umri na wanakotoka katika mabano ni Hassan Ally Tarimo (38- Moshi Mjini), Agness Costantine (43-Singida Mjini), Alex Godii (45 - Mererani, Manyara), Masinyari Nuhu (80 - Engaruka, Monduli), Daudi Shanu (31 -Moshi), na Holo
Nigha (40 - Kishapu, Shinyanga).
Wengine ni Grace Somi (59 -Moshi Mjini), Eva Sumaye (65 - Lekamba, Arusha), Hadija Wambura (30 - Tarime, Mara), Juma Ally (45 - Tanga), Fatuma Shaban (54 - Ngara, Kagera), Mrs Moshi (60 - Msagara, Moshi), Donald Msele (47 - Misungwi, Mwanza) na Mama Ndossi (70 - Bomang'ombe, Moshi). Wengine ni Okonbo Oguyi (78 - Musoma Vijijini), Stella Hagai (43 - Dar es Salaam), Diana Munisi (20 -Hai, Moshi), Flora Assenga (42 - Chumbageni, Tanga), Steward Mgosingwa (86 -Muheza, Tanga), Shanuel Mushi (22 - Lyamungo, Hai), Penina Wiga (38 - Shirati, Rorya) na Mwajuma Ramadhani (72 - Dodoma Mjini).
Margaret (35 - Rorya, Mara), Eliashenya Bilingi (78 - Meru), Steven Haule (53-Majengo, Tabora), Mary Sindani (38 - Manyoni, Singida), Ngangi Nana (70-Milima Meru), Kabula Kazungu (24 - Nyanguge, Magu), Elizabeth Emmanuel (74 - Arusha) na Jaston Kusoma (35 - Katesh).
Norbert Kudome (33 - Moshi), Philipo Jalo (35 - Mwanza), Stella Mwanyemba (42 -Busali, Kyela), Haikaeli Msocha (62 -Mlalo, Lushoto), Joy Rose (36 - Msanga, Chamwino), Hamis Kazyoba (70 - Kahama, Shinyanga), Mjaledi Munka (65 - Makete, Iringa), Esther Rutainyu (49 - Biharamulo) na Mwanahamis Rajabu (32 - Tabora Mjini).
Katika orodha hiyo pia wamo, Mwanaisha Isaka (70 - Dodoma Mjini), Rehema Sadalla (30 - Kiteto, Manyara), Emmanuel Napengwa (68 - Ilala, Dar es Salaam), Amina Kimweri (62 - Makanara, Korogwe), Butondo Mbuje (26 - Manyoni, Singida), Elise Mandari (76 - Mamba Kusini, Moshi), Jonathan Mnyiremi (Sorya, Manyoni) na Elisaria Urio (50 - King'ori Arumeru).
Wengine ni Shafu Muya (30 -Korongoni, Moshi), Paschal Shaghembe (47 - Geita Mjini), Bertha Muro (78-Machame, Hai), Lucas Machimo (56 - Ugogoni, Korogwe), Magdalena Kalole (35- Kimara, Dar es Salaam), Charya Mashishi (45 - Usanga, Maswa), Josephine Robert (34-Murukurazo, Ngara), Asha Nkinda (65 -Tanga Mjini) na Lyidia Msuya (78 - Kimara, Dar es Salaam).
Wagonjwa wengine waliofariki ni Paulina Portea (65 - Ganako, Karatu), Alemwene Mwakatobe (69 - Mwanjelwa, Mbeya), Marieta Mandwa (56 - Shinyanga), Masalu Nhelegani (65-Nyangokolo, Bariadi), Emmanuel Mang'arai (56 - Arusha), Amina Chuwa (86 - Uru, Moshi), Eliadi Mariki (40 - Mwika, Moshi Vijijini) na Mmoja Juma (25 - Bukumbi, Tabora).
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwananchi lilishuhudia baadhi ya watu katika Kijiji cha Samunge wakiwa wamebeba maiti ya mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Rukia Rajab, Mkazi wa Kondoa wakati majina ya watu wengine wanne waliofariki dunia bado hayajatambuliwa.Kadhalika, mmoja wa maiti ambazo majina yake hayakutambuliwa alifahamika kuwa ni mkazi wa Biharamulo, mkoani Kagera.
Sababu za vifo
Lusasi alisema kwa mujibu wa taarifa za madaktari, vifo vingi vimesababishwa na magonjwa ya kisukari, pumu na shinikizo la damu. "Wagonjwa wengine walikuwa wakifika Samunge unamwangalia na kumwona kuwa huyu alikuwa amewekewa drip, lakini yuko pale akiwa kwenye foleni akisubiri kwenda kwa Mchungaji kunywa dawa," alisema Lusasi na kuongeza:
"Sasa katika hali hiyo kama mgonjwa ni wa kisukari, wengi walipoteza maisha kwani hata vyakula walivyokuwa wakila pengine havikuwa vikikidhi matakwa ya ugonjwa husika."Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, waliimarisha huduma za afya katika Zahanati ya Kijiji cha Samunge kwa kuongeza watumishi wa afya na dawa za magonjwa hayo lakini akasema watu walikuwa hawajitokezi hadi pale hali zao zilipozidi kuwa mbaya.
Alisema zahanati hiyo pia imekuwa ikipewa mgawo mkubwa wa dawa nyingine kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na idadi ya wagonjwa kuongezeka.Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa siku kadhaa umebaini kuwa baadhi ya wagonjwa walichukua dawa za siku chache wakitaraji kwamba wangetumia muda mfupi kupata kikombe cha Babu, lakini kinyume chake walijikuta wakikaa kwenye foleni kwa muda wa kati ya siku saba na kumi na moja.
Kutokana na kuwapo kwa dalili za tiba ya Mchungaji Mwasapila kuendelea kwa muda mrefu, Lusasi alisema Halmashauri ya Ngorongoro inakusudia kujenga chumba kidogo cha kuhifadhia maiti katika Zahanati ya Samunge ili kukabiliana na tatizo la maiti kuzikwa kabla ya ndugu zao kufika kuwachukua.
Alisema sababu nyingine iliyochangia vifo hivyo ni kuzibwa kwa barabara kiasi kwamba gari la wagonjwa lililopelekwa na halmashauri kushindwa kuwasadia wale waliokuwa wamezidiwa."Gari lile mara kadhaa lilijaribu kupenya, lakini lilishindwa kutokana na watu kukataa kulipa nafasi, tulijaribu kila njia, kuweka mabango kwenye gari, kuweka bendera na hata kutumia kipaza sauti kutangaza lakini ilishindikana," alisema Lusasi.
Habari hii ni kwa hisani ya
Mwananchi.co.tz
Habari hii ni kwa hisani ya
Mwananchi.co.tz
No comments :
Post a Comment