Benki
Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti
halali (legal tender) zinazotumika nchini. Katika kutekeleza jukumu hili
Benki Kuu hutengeneza noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani
(denominations) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa
kuweza kugawika katika zile zenye thamani ndogo ndogo.
Hii
hulenga kurahisisha upatikanaji wa chenji na uwezekano wa wahitaji wa
viwango mbalimbali vya bidhaa na huduma kupata katika mafungu
yatakayokidhi mahitaji yao.
Katika kutekeleza jukumu hili, Benki Kuu imetoa toleo jipya la Sarafu ya Shilingi 500. Hatua hii imezingatia yafuatayo:
• kwamba
noti ya shilingi mia tano (500), ndiyo inayotumika zaidi kwenye
manunuzi ya kawaida ya kila siku ya wananchi wengi kuliko noti nyingine
yoyote. Hivyo noti hiyo hupita kwenye mikono ya watu wengi katika
kipindi cha muda mfupi sana na kuchakaa haraka.
• Noti
hizi hukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye
mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe zinapokuwa zimefikia ukomo
wake.
• Sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi kuliko noti.
Sarafu hii inatambuliwa kwa kuangalia yafuatayo:
• Umbo lake ni la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5
• Ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma (Steel) na “Nickel”
• Kwa
mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa
mbugani.
• Ina
alama maalum ya usalama iitwayo “latent image” iliyopo upande wa nyuma
ambayo ni kivuli kilichojificha. Kivuli hiki huonesha thamani ya sarafu
‘500’ au neno ‘BOT’ inapogeuzwa-geuzwa.
Sarafu hii mpya ya shilingi mia tano (500) inatarajiwa kuingizwa kwenye mzunguko kuanzia mwezi Oktoba 2014. Sarafu
hii, itakuwa ikitumika sambamba na noti zilizopo sasa za shilingi mia
tano mpaka hapo noti hizo zitakapokwisha katika mzunguko. Pamoja
na taarifa hii; tunawaomba wananchi kuendelea kufuatilia vipindi
mbalimbali vitakavyokuwa vinaeleza jinsi sarafu hii ilivyo na namna ya
kutunza noti na sarafu zetu kwa njia salama.
Ahsanteni Sana
Mkurugenzi
Huduma za Kibenki kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw. Emmanuel
Boaz(wa kwanza kulia) akiwaeleza waandishi wa habari(Hawapo Pichani)
sababu zilizopelekea kutoa toleo jipya la sarafu ya shilingi 500, ambapo
alisema noti ya shilingi 500 inatumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida
ya kila siku hivyo hupita kwenye mikono ya watu wengi na kuchakaa
haraka,noti hizi hukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa
kwenye mabenki na sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa muda mrefu kuliko
noti. Katikati ni Mshauri wa Fedha kutoka ofisi hiyo Bw. Hassan Jarufu
na Mwisho ni Meneja Msaidizi, Sarafu Bw. Abdul Dola.
No comments :
Post a Comment