SI
UTANI; nimesema siitaki Tanzania ambayo viongozi na Watawala wake
hawataki kuimba wimbo wa, Ili Tuendelee, tunahitaji vitu vinne; Watu,
Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora.
Kiongozi
lazima atokane na Watu, wasipokuwepo watu hakuna Kiongozi, ataongoza
Mawe? Kiongozi asiyejali watu si Kiongozi; Hivyo siitaki Tanzania
itakayoruhusu watu wake wauawe ovyo kama ndege, watekwe, wajeruhiwe na
kuwindwa kama Wanyama au ndege.
RASHID KAWAWA |
Siitaki
Tanzania ambayo Viongozi wake hawatajali Uridhi wa Vizazi vya watu wake
ikiwemo Ardhi. Mtawala atakayeacha watu wake wanyang’anywe na
kudhulumiwa Ardhi, huyo hawapendi watu wake na wala hatokani nao. Watu
wanaweza kukusaidia.
Sitaki
hata kuiona Tanzania yenye siasa Chafu, Siasa ya Kuhasimiana, ya
kulipizana Visasi, Siasa ya kumfurahisha mtu na kuwaumiza wengine, ya
Kung’angania Madaraka, Siasa ya Nyangumi, Mamba na ya Sumu ya Nyoka.
Sipendi
kunusa, kuiona hata kuisema, Siasa ya kuviziana, kutekana na Kutupana
Mabwepande, kutoana Meno, Kucha, kutoboana Macho, Kumwagiana Tindikali,
ya Mabomu ya Machozi, Siasa ya Maji ya Kuwasha.
Kama
Siasa ya namna hiyo itaendelea kujiri; ni heri kuishi chini ya Mkoloni,
ni heri tusigambe kuwa tuna Uhuru, na ni Kheri tuitwe wanyama kama
walivyotuita Wazungu, kwamba tu Masokwe watu, kutokana na tabia hiyo ya
kutesana wenyewe!
Naichukia
sana Siasa ya Makundi na Usultani, inayodharau watu wengine na
kuwafanya waonekane kama Kinyaa, kiasi cha kuwaita huzungumzi na Mbwa,
ila Mwenye Mbwa! Maana kama kilichoumbwa na Mungu kikapuliziwa Pumzi ya
Uhai ni Mbwa!.........
Sithubutu
kuinusa hata kuipa Mawazo Siasa ya wasiokubali kushindwa, wanaoona wako
sawa, hata wanapokosea, wanaoona pekee yao ndio wanafaa kutawala, kumbe
hata uwezo wa kutawala hawana! Wanaotaka wasikilizwe wao tu! Wao
wasisikilize!
Natamani
Mungu angerejesha, Utawala wa Tanganyika ambao ndani mwake alikuwemo
Baba wa Taifa na Mwasisi wake Mwalimu Julius Nyerere, ambapo tulionekana
kama tunachelewa lakini tuliheshimiwa! Na watu waliishi miaka Mingi!
Naitaka
Tanganyika hiyo iliyokuwa haina Ufisadi, tofauti na wa leo wa
kupindukia. Siku hizi anaweza akauawa Mtu mchana kweupe na watu wanaona
na Polisi wakishuhudia ukiporwa kila kitu, lakini wasiseme chochote!
Naipenda
Tanganyika ya Bibi Titi Mohamed, ambayo ilikuwa haina Udini, iliyovaa
Utu! Uadilifu na Uzalendo wa Taifa hili. Naitaka Tanganyika ya Waziri
Mkuu Rashid Mfalme Kawawa (Simba wa Yuda), ambaye hata akikosolewa
alikuwa anakubali!
BIBI TITI |
Naitaka
Tanganyika ya waliosema, Madini ardhini hayaozi hadi wazao wao wapate
Akili na vifaa vya kuvunia yakiwa nchini Tanganyika, kuliko kukodi watu
wayachimbue kwa madai watu wetu hawana uelewa lakini yanatoroshwa na
kuwapa faida wageni.
Siitaki Tanzania ya Viongozi wanaochaguliwa kwa Rushwa na Ufisadi, wanaochukia wandishi ambao
wakiwa madarakani wanarudisha kwanza fedha walizotumia kupata Uongozi,
na hatimae kuwakumbuka Watanganyika kwa kuwabagua kwa Udini, na
kurithishana Uongozi Kiu-koo.
Pia
Sitaki hata kusikiliza, Bunge la Tanzanaia ya Leo, ambalo wabunge
wake wanasema Ndiyooo! hata kwenye Elimu Chafu! hawaungani kusema siyo
kwenye siyo na ndiyo kwenye Ndiyo kama Enzi ya Tanganyika ya Spika Adamu
Sapi Mkwawa.
Siitaki
Tanzania ya Viongozi wanaotuhumiwa kuwa na Vyeti Bandia, au
vilivyoungwaungwa kama Nywele Bandia za kuunganisha, ilihali zenyewe ni
za Kipilipili, na wanaoporomosha Matusi bungeni kama Mabomba ya Maji.
Makala hii imeandikwa na
Makala hii imeandikwa na
nyeregete@yahoo.co.uk 071593308
No comments :
Post a Comment