Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda- Maelezo, Bagamoyo
Wanafunzi
wa shule za Sekondari wilayani Bagamoyo wametakiwa kusoma kwa bidii na
kufanya vizuri kwenye mitihani
yao kwa kufanya hivyo wataweza kufanikiwa katika maisha yao kwani
elimu ni mkombozi wa maisha ya binadamu.
Mwito huo umetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete wakati
akiongea kwa nyakati tofauti na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya
Mandera na Mboga zilizopo wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete alisema kama wanafunzi hao watasoma na kufanya
vizuri katika mitihani yao wataweza kufanikiwa kimaisha, watapata kazi na
kuwasaidia ndugu zao na hivyo kupunguza tatizo la umaskini ndani ya jamii
zao.
“Mjenge tabia ya kusoma kwa makundi msione fahari
kukaa nyumbani hasa mwisho wa wiki tumieni muda wenu wa ziada
kusoma kwa pamoja , mchague viongozi wa makundi na kila mmoja wenu
awe na somo la kuwafundisha wenzake hii itasaidia kila mtu kufaidika na
mwenzake”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaasa wanafunzi wa kike
kutokubali kudanganywa na wanaume na kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi
wangali wanafunzi kwa kufanya hivyo watapata mimba zisizotarajiwa na ugonjwa wa
Ukimwi hivyo kukatisha masomo yao na kutotimiza ndoto zao .
Alionya, , “Msikubali kudanyanywa na wanaume na
kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wakati uko shule hata kama mzazi wako
hana hela za kutosha za kukupatia usikimbilie kwa mwanaume bali unaweza
ukatumia kipindi cha likizo kufuga kuku wa asili na unaporudi shuleni unawaomba
walezi wako wanakuangalizia kuku hao wakikua utawauza na kujipatia pesa”.
Mama Kikwete pia aliwaasa wanafunzi hao kuvaa mavazi
ya heshima na kujiheshimu na kuacha kuiga mambo ambayo hayawasaidii katika
maisha yao ambayo yanaonyeshwa katika Televisheni bali wapambane katika
masomo ili waweze kufanikiwa katika maisha yao na kama wataona wenzako
hawahudhurii darasani kwa ajili ya utoro wawakanye.
Kwa upande wa walimu aliwata kuwalea wanafunzi hao
kama kama watoto wao wa kuwazaa kwani wao ndiyo wanadhamana kubwa katika malezi
ya wanafunzi.
Aidha Mama Kikwete alitumia muda huo kuwataka
wanafunzi hao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Dengue ambao na
hauna kinga na unaenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae ambaye hupenda
kuuma watu nyakati za mchana.
“Chukueni hatua dhidi ya ugonjwa huu kwani unaua watu
kwa kusafisha mazingira na kuua mazalia yote ya mbu kwani mbu huyu mazalia yake
ni maji masafi meupe yaliyotuama pia huweza kuwepo hata ndani ya nyumba.
Alizitaja dalili za ugonjwa huo ni kuumwa kichwa,
maumivu ya viungo na uchovu, homa kali, dalili hujitokeza siku ya tatu hadi ya
14 tangu kuambukizwa na kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed
Kipozi alimshukuru Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya na moyo alio
nao wa kuwalea na kusimamia elimu ya watoto wa kike jambo ambalo linawapa nguvu
watendaji wa Serikali na kuwapa moyo wanafunzi ambao wapo katika
safari ya kujijengea maisha yao ya baadaye.
Akisoma taarifa ya Shule ya Sekondari ya wasichana
Mandera Mkuu wa Shule Rose Umila alisema shule hiyo ina wanafunzi 428 wa kidato
cha kwanza 144, cha pili 107, cha tatu 84 na cha nne 93 na walimu 22 kati ya
hao walimu wa wasanaa 17, biashara mmoja na sayansi wanne.
Mwalimu Umila alisema, “Kwa upande wa taaluma bado
tuna changamoto ya wanafunzi kutofanya vizuri sana ukilinganisha na matokeo ya
mwaka juzi ingawa tulijitahidi kupunguza daraja la sifuri.
Tatizo kubwa lilikuwa ni upungufu wa walimu pamoja na
wanafunzi kutokuwa makini kwenye masomo yao, wanafunzi kuchelewa kurudi
kutoka likizo fupi na ndefu hata kwa wale wanaofadhiliwa na mashirika kama
CAMFED na wale wanaotoka katika kijiji cha Mandera wanachelewa kurudi bila
sababu yoyote”
Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na
uhaba wa mabweni, ukosefu wa bwalo la chakula, walimu ya Fizikia na
Hisabati, nyumba za walimu na shule kutokuwa na usafiri ni tatizo hasa pale
wanafunzi wanapoogua ghafla na hasa usiku kwani huduma inapatikana Hospitali
ya Miono.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Mboga George
Elias alisema Shule hiyo ni shule ya kata ya Msoga inajumla ya wanafunzi 273
kati ya hao wavulana ni 162 na wasichana 111, walimu 23 na watumishi wasio
walimu wanne.
“Tunakabiliwa na tatizo la kuripoti kwa
wanafunzi wanaopangwa kuanza kidato cha kwanza , uongozi wa Shule na Kata
unashirikiana kwa karibu kudhibiti suala zima la kutoripoti na utoro wa
wanafunzi Shuleni kutokana na matatizo hayo wapo wazazi waliofikishwa
Polisi na Mahakamani”, alisema Mwalimu Elias.
Alisema kutokana na idadi ya wanafunzi na mikondo
iliyopo ambayo ni sita hakuna upungufu wa vyumba vya madarasa kwani wanavyumba
saba lakini kulingana na mpango wa maendeleo wa shule bado kuna upungufu
wa majengo.
Changamoto zingine ni upungufu wa vitabu, vifaa vya
michezo, walimu wa Sayansi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vifaa vya
mabara, kutokuwa na nyumba za walimu na kutokuwa na nishati ya umeme.
Mama Kikwete ni Mlezi wa Shule ya Sekondari ya wasichana
Mandera na katika shule ya Sekondari Mboga anawalea wanafunzi wa kike. Akiwa
katika shule hizo aliwapatia zawadi za vyakula kama mchele, maharage, unga wa
ugali, mafuta ya kupikia, sukari, majani ya chai, vyombo vya kupikia
ikiwa ni pamoja na majiko, masufuria na vyombo vya kulia vyakula ambavyo ni
sahani, vijiko, vikombe, majagi, majaba ya kuhifadhia maji na kandambili.
No comments :
Post a Comment