Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge
anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali
(PAC). Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za
Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC ni
kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za
umma katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni
baadhi tu ya Mashirika ya Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa
PAC.
Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia
makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd. na Gombe Advisors Ltd., amefanya
biashara na TANAPA, shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na
Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki washirika wake,
kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd.,
wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya
ukiukwaji wa Sheria uliofanywa na viongozi wa umma na mashirika ya umma
katika kashfa hii. Pamoja na maelezo yatayotolewa , Kambi Rasmi ya
Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya
ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na TANAPA na NSSF;
msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo kwa
kuzingatia masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika
usimamizi wa fedha za umma.
Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa
kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria
nyingine zinazohusika. Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu
mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa
fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye
uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya
Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya
kiongozi wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji wa maslahi.
No comments :
Post a Comment