Meneja
Masoko wa Shirika la Posta Tanzania Bw. David George akiwaeleza
waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es salaam kuhusu
mafanikio yaliyofikiwa na shirika hilo hadi sasa ikiwemo kuanza kutumika
kwa anuani za makazi na Misimbo ya posta (Post code) inayolenga
kuboresha huduma za shirika hilo,kulia ni Kaimu Meneja huduma za barua
Bw.Jason Kalile.
(Picha na Idara ya Habari Maelezo)
Frank Mvungi- Maelezo
Shirika la Posta Tanzania
linatarajia kuanza kutoa huduma zake kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa
anuani za Makazi na Misimbo ya Posta kabla ya Mwisho wa Mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Meneja Masoko
wa Shirika hilo Bw. David George wakati wa mkutano na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua David amesema kuwa kwa
kuzingatia mpango kazi wake shirika hilo limedhamiria kufikia mwakani
nusu ya Mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani iwe imefikiwa na huduma ya
anuani za Makazi na Msimbo wa posta.
Aidha David amesema kuwa huduma
hiyo tayari imeanza kutolewa katika Mikoa ya Arusha ambapo imehusisha
kata 8, Dodoma kata 8, na Dar es salaam hadi kufika June 2014 kata 27
zitakuwa zimefikiwa ambapo lengo kuu ni kuboresha huduma na kufikisha
barua pamoja na vifurushi katika makazi ya wateja kwa wakati.
Pia David alieleza kuwa Shirika
hilo lina mpango kabambe wa kuleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji
na utoaji huduma za Posta nchini ili kunufaika na fursa zinazoletwa na
mabadiliko ya teknolojia,kuboresha huduma,kukidhi mahitaji ya soko na
kukabiliana na ushindani.
Akifafanua Bw. David amesema lengo ni na kuongeza tija kwa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa.
Shirika la Posta Tanzania
linatekeleza mpango wa miaka 10 ( 2014-2023) unaozingatia juhudi kubwa
zinazofanywa na Serikali kupitia utekelezaji wa sera na mipango
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Dira ya maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa
Matokeo wakubwa sasa,sera ya posta 2003,Mkakati wa kukuza uchumi na
kupunguza umasikini (MKUKUTA),Mpango wa kurasimisha rasilimali za
biashara za wanyonge (MKURABITA),Mfuko wa Taifa wa anuani za Makazi na
Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA.)
No comments :
Post a Comment