Ushirikiano
wa pamoja unatakiwa baina ya wanafunzi, walezi, wazazi, jamii na walimu
ili kuweza kujenga, kuimarisha na kukuza nidhamu , mwenendo na tabia ya
mtoto jambo ambalo litaleta mafanikio chanya pamoja na kutatua
changamoto za kitaaluma na kimazingira.
Hayo
yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na
walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Salma Kikwete iliyopo
kata ya Kijitonyama wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema nidhamu ya mwanafunzi siyo tu kumuamkia mwalimu bali pia
kujua wajibu wake kama vile kuwahi shuleni, kufanya mazoezi ya darasani
na kusoma kwa bidii.
“Neno
nidhamu lina dhana pana kwani linagusa wengi lakini katika mazingira ya
leo walengwa wakubwa ni mzazi,mlezi au jamii, mwalimu na mwanafunzi.
Kazi ya mzazi, mlezi na jamii ni kuhimiza na kufuatilia maendeleo ya
mtoto.
Mwalimu
kufundisha, kuingia darasani kwa wakati na kujiandaa na kwa
mwanafunzi ni kupokea maarifa anayopewa na mwalimu wake na kusoma kwa
bidii”, alisema Mama Kikwete.
Kwa
upande wa wanafunzi aliwasihi kuongeza juhudi katika masomo na kufanya
vizuri kwenye mitihani, kwani wao na wengine wote wanategemewa na
familia, jamii zao na taifa kwa kuwa watakuwa wakombozi siku za baadaye
na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na ujasiri katika safari yao
ndefu ya kufatuta elimu.
Aidha
Mama Kikwete aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa kazi kubwa
wanayoifanya ya uboreshaji wa elimu pamoja na kukabiliwa na changamoto
kadhaa lakini kadri siku zinavyokwenda mbele ndivyo Serikali inavyozidi
kutatua changamoto mbalimbali zinazowahusu walimu.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisisitiza, “Walimu timizeni wajibu wenu kwa kufika
kazini mapema, kumaliza silabasi kwa wakati, kukamilisha maandalio ya
masomo, kufundisha kila kipindi bila kukosa, kujua taarifa na udhaifu wa
wanafunzi wenu na kuwa kiungo kati yenu na wazazi au walezi
hiyo ndiyo nidhamu ya mwalimu na ndiyo ualimu”.
Akisoma
taarifa ya shule hiyo Mwalimu Elestina Chanafi alisema shule hiyo
ilianza mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 320, walimu 13 na vyumba vya
madarasa sita hivi sasa ina wanafunzi 1229, walimu 33 na vyumba vya
madarasa 22. Hadi sasa jumla ya wanafunzi 1161 wamehitimu masomo yao
tangu walipoanza kutoa kidato cha nne mwaka 2010.
Mwalimu
Chanafi ambaye ni Mkuu wa shule hiyo alisema wamefanikiwa kuchimba
kisima cha maji kwa msaada wa wakorea, kuunganisha umeme, kununua vifaa
mbalimbali vya uchapaji na udurushaji, kuboresha mazingira kwa kiwango
cha kutia moyo na kuweza kuwavutia wanafunzi ili wajisikie kuwa sehemu
ya shule.
Kuanzisha
maabara ya muda ambayo imewawezesha wanafunzi wa sayansi kufanya
mitihani kwa vitendo na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa masomo hayo na
kupata wanafunzi wa kujiunga na masomo ya ngazi ya juu kwa idadi nzuri.
“Changamoto
zinazotukabili ni uchakavu wa baadhi ya vyumba vya madarasa, mmomonyoko
mkubwa wa maadili ambao unasababisha ugumu katika kudhibiti nidhamu ya
wanafunzi, uelewa mdogo wa wazazi juu ya mchango wao kwa maendeleo ya
wanafunzi, kiwango kidogo cha ruzuku toka Serikalini ambacho hakiletwi
kwa ukamilifu na wakati, ufinyu wa bajeti na ulegevu wa uchangiaji wa
ada na michango mingine toka kwa wazazi”, alisema Mwalimu Chanafi.
Naye
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana alimshukuru Mama Kikwete
kwa kupata nafasi ya kuitembelea shule hiyo na kumpongeza kwa kazi
anayoifanya ya kuinua kiwango cha elimu nchini na kuendeleza fani yake
ya ualimu kwa faida ya kizazi cha leo na kijacho kwa kuwasomesha watoto
zaidi ya 600 hawa ni mbali na wanafunzi walioko Shule ya Sekondari
WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Mama
Kikwete aliichangia shule hiyo mifuko 100 ya simenti ambayo itatumika
kuzima mashimo katika vyumba vya madarasa ambapo wilaya ya Kinondoni
itagharamia mchanga pamoja na kumlipa fundi atakayefanya kazi hiyo.
No comments :
Post a Comment