Kampuni
ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania leo imeipiga jeki timu ya taifa
ya Netiboli - Taifa Queens kwa kuipatia vifaa mbalimbali vya michezo
vyenye thamani ya shilingi milioni sita kuiwezesha timu hiyo kushiriki
vema mashindano ya Afrika yanayoanza kesho jijini Dar es salaam.
Vifaa hivyo ni suti za michezo jozi 20, viatu vya michezo jozi 20, jezi seti mbili, BiBs 20 vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni Sita na kukabidhiwa leo kwa Mke wa Waziri Mkuu Tunu Pinda kutoka kwa Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Vodacom Tanzania Bw Salum Mwalim katika hafla fupi iliyofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam.
Akipokea vifaa hivyo Mama Pinda ameishukuru Vodacom kwa kuunga mkono juhudi za kuyawezesha mashindano hayo kufanyika vema chini ya uenyeji wa Tanzania kupitia chama cha Netiboli nchini – CHANETA.
“Nawashukuru sana Vodacom mmetupatia zaidi ya kile tulichowaomba, hii sasa ni wazi timu yetu ya Taifa Queens itafanya vizuri na kuibuka mshindi wa mashindano hayo makubwa kwa netiboli Afrika”Alisema Mama Pinda.
Kwa upande wake Bw. Mwalim alimpongeza Mama Pinda kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mashindano hayo yanafana chini ya ardhi ya Tanzania.
“Kwa kweli mama umefanya kazi kubwa na nzuri sana inayostahili kila aina ya pongezi ya kuzunguka kila mahali kuhamasisha watanzania kuyachangia mashindano haya na timu yetu ya taifa – Taifa Queens, hakika umeonesha mfano mzuri na wa kuigwa kwamba Netiboli ikisimamiwa kidete kama ulivyofanya nayo chati yake itakuwa juu”Alipongeza Bw. Mwalim.
Bw. Mwalim aliongeza kusmea kuwa Vodacom siku zote inajivunia ushiriki wake katika kukuza michezo nchini ikitambua kuwa michezo ni eneo muhimu la kuwaunganisha watanzania na kuwapatia wakati wa furaha baada ya pirika za hapa na pale.
“Vodacom tunajivunia rekodi yetu ya kuendeleza na kukuza michezo nchini leo taifa zima linapongezana na kupena pole kufuatia mechi ya jana ya Simba na Yanga hayo ni matunda ya Vodacom kuweka udhamini katika soka na leo tunajivunia kuiwezesha Taifa Queens kushiriki mashindano ya kimataifa”Alisema Bw. mwalim
No comments :
Post a Comment