Kikosi cha Stars Mechi ya kwanza mchujo ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) iliyochezwa jana (Julai 13 mwaka huu) imeingiza sh. 113,268,000 kutokana na watazamaji 17,121. |
Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo
wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT) ni sh. 17,278,169.49 wakati wa gharama za uchapaji
tiketi ni sh. 7,809,104.
Asilimia
15 ya uwanja sh. 13,227,108.98, asilimia 20 ya gharama za mechi sh.
17,636,145.30 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
sh. 4,409,036.33.
Asilimia
60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 52,908,435.91 na
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,645,421.80
ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
TAIFA STARS KAMBINI TENA JULAI 4
Timu
ya Taifa (Taifa Stars) imeondoka leo asubuhi (Julai 14 mwaka huu)
kwenda Mwanza ambapo itapiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi ya
marudiano dhidi ya Uganda (The Cranes) kutafuta tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani
nchini Afrika Kusini.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeondoka kwa ndege ya
PrecisionAir na itafikia hoteli ya La Kairo wakati mazoezi yatafanyika
Uwanja wa CCM Kirumba kulingana na programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen.
Wachezaji
walioko katika kikosi hicho ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini
Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub
Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri
Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vincent Barnabas,
Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.
Mechi
ya marudiano itachezwa kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu kwenye Uwanja
wa Nelson Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala. Tarehe
rasmi itapangwa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Uganda
(FUFA) siku kumi kabla ya mechi.
TENGA AWASHUKURU WAJUMBE WA MKUTANO MKUU TFF
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa michango yao, na utulivu
waliouonesha katika kupitisha marekebisho ya Katiba ya TFF ya 2013.
Amesema
marekebisho hayo yatawasilishwa kesho (Julai 15 mwaka huu) kwa Msajili
wa Klabu na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kupitishwa ili mchakato wa
uchaguzi uweze kuanza mara moja.
“Tutamuomba
Msajili atusaidie kusajili haraka Katiba yetu ya 2013 ili tuingie
katika mchakato wa uchaguzi. Kama tulivyotangaza awali tumepanga kufanya
uchaguzi Septemba 29 mwaka huu, na tusingependa tarehe hiyo ipite,”
amesema Rais Tenga wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada
ya kikao cha Kamati ya Utendaji.
Katika
kikao chake, Kamati ya Utendaji imepitisha Kanuni za Maadili, Kanuni
za Nidhamu, na marekebisho kwenye Kanuni za Uchaguzi yanayotokana na
kuundwa kwa Kamati ya Maadili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments :
Post a Comment