Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wassira akizungumza kwenye mdahalo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema) Tundu Lissu na katikati ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba. Picha na Rafael Lubava.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira akiwakilisha CCM, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, jana walitoana jasho katika mdahalo wa Katiba ulioandaliwa na East African Business and Media Institute.
Mdahalo huo uliohudhuriwa na watazamaji wapatao 500, ulikuwa na mada inayosema: ‘Nani anakwamisha Upatikanaji wa Katiba Mpya.’ Kila upande ulitumia fursa hiyo kutupa shutuma kwa mwingine huku jazba na kelele vikitawala miongoni mwa waliohudhuria.
Hata hivyo, suala la muundano wa serikali ndiyo uliochukua nafasi kubwa katika mdahalo huo huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukiishutumu Serikali ya CCM kuwa ndiyo kikwazo cha upatikanaji wa Katiba Mpya nayo ikitupa mpira huo kwa Ukawa kwa kitendo chake cha kutoka katika Bunge Maalumu la Katiba.
Profesa Lipumba alisema wahafidhina wa CCM ndiyo waliomshauri Rais Jakaya Kikwete abadilike kimsimamo kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya.
“Rais Kikwete alikuwa na nia njema kabisa kuhusu Katiba Mpya lakini wahafidhina wa CCM wanaopenda madaraka walipoona muundo wa serikali tatu wakambana naye akabadilisha msimamo, tunamwomba abadilike, nchi hii ni yetu sote ili tupate katiba ya wananchi,” alisema.
Lissu aliongeza kwa kusema kuwa anayekwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni CCM ambao wanaweka maoni yao badala ya kujadili rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo maoni ya wananchi.
“Hatuwezi kurudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwenda kujadili rasimu ya CCM kwa sababu wanaonyesha hawana nia ya Katiba Mpya, bali wanataka kuwadanganya Watanzania, watawadanganya wananchi kwa kuleta Katiba ileile ila ikiwa na rangi tofauti,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema Ukawa hawawezi kushiriki katika udanganyifu wa aina hiyo na kwamba wameamua kuwaachia CCM ili wananchi waweze kuwahukumu kwa uovu watakaoufanya.
Alisema kati ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika Kundi la 201, wajumbe 166 ni wana CCM walioteuliwa ili kuongeza idadi ya watu.
“Humo kuna viongozi wa dini mashehe na maaskofu na waganga wa kienyeji ambao ni wana CCM ili wapitishe Katiba yenye masilahi yao binafsi,” alisema.
Hata hivyo, Wassira alisema hoja za Ukawa hazina mashiko na kumtaka Lissu kuwaomba radhi masheikh na maaskofu kwa kuwa hawakuteuliwa na Rais kutokana na kuwa wanachama wa CCM, bali ni mapendekezo ya taasisi wanazozitumikia.
“Namwomba Tundu Lissu akawaombe radhi masheikh na maaskofu kwa sababu kundi hili liliteuliwa kutokana na mapendekezo ya wahusika wenyewe pasipo shinikizo la Rais. Hapakuwa na uwezekano wa Rais kuwatambua wana CCM ili awateue wanaofaa. Kama ana ugomvi na Kingunge Ngombale Mwilu aseme.”
Alisema wanaokwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni Ukawa... “Katiba Mpya haiwezi kupatikana mitaani, bali kwa majadiliano na maridhiano kwenye Bunge Maalumu la Katiba, nawashauri warudi bungeni ili tuweze kupata Katiba Mpya.”
Alisema Bunge Maalumu la Katiba lina mamlaka ya kubadilisha vifungu kwenye rasimu ya Katiba na kwamba halipo kwa ajili ya kupitisha tu vifungu vilivyowekwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo ya Wassira ilifanya kila aliposimama kuzomewa na wananchi waliohudhuria mdahalo huo huku wafuasi wa Chadema na CCM wakitishiana kupigana hali iliyosababisha mabaunsa kuwatoa nje ya ukumbi baadhi yao walioshindwa kustahimiliana.
Wajumbe wawili waliokuwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole na Awadh Said, katika michango yao walitaka kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi ili kupata katiba itakayowafaa kwa muda uliokusudiwa.
Polepole alisema tatizo la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni masilahi binafsi na ya makundi katika utafutaji wa Katiba Mpya.
“Wananchi wasimamie masilahi ya taifa na wasiwaachie mchakato mzima wanasiasa ambao wana masilahi binafsi pamoja na yale ya kikundi yenye shinikizo la masilahi binafsi,” alisema Polepole.
Awadh alisema maoni yalikusanywa kutoka katika mabaraza ya katiba 170 na 600 ya taasisi na vyama vya siasa kutoka katika wilaya zote 43 za Zanzibar.
“Kwa nini juhudi zote hii zibadilishwe na wajumbe 629 peke yao kwenye Bunge Maalumu la Katiba? Tufuate maoni ya wananchi kupitia tume ndipo tutakuwa tunawatendea haki Watanzania,” alisema.
Alielezea kusikitishwa na kitendo cha Serikali kufunga tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba akisema kimewanyima wananchi haki ya kupata taarifa mbalimbali za tume hiyo.MWANANCHI
No comments :
Post a Comment