Na. M. M. Mwanakijiji .
Mpigania
haki za weusi na alama kuu ya udhalimu wa mfumo wa Ubaguzi wa Rangi
nchini Afrika ya Kusini Mzee Nelson ‘Madiba’ Mandela amefariki dunia
baada yakuugua kwa muda mrefu kufuatia maambukizi ya mapafu kushindwa
kutengemaa kwa muda sasa. Mzee Mandela ambaye kwa miezi kadhaa sasa
amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya maambukizi kwenye mapafu yake
amefariki dunia nyumbani kwake ambako alipelekewa toka hospitali ya Moyo
ya Mediclinic mjini Pretoria, chini Afrika ya Kusini baada ya familia
yake kuomba kufanya hivyo.
Mzee
Mandela alipelekwa hospitali hiyo Jumamosi ya tarehe 8 Juni ikiwa ni
baada ya kuanza tena kusumbuliwa na mapafu; miaka ya themanini akiwa
kifungoni Mandela alipata ugonjwa wa Kifua Kifuu (TB) kutokana na kazi
ngumu ya kupasua mawe kama sehemu ya adhabu ya kifungo chake. Aliondoka
hospitali hapo Septemba 1, 2012 baada ya familia kuomba hivyo na
kuahidiwa huduma nzuri ya kitabibu nyumbani. Wakati anaondoka hospitali
hali yake bado ilikuwa ya utulivu kidogo lakini isiyo na mabadiliko
makubwa. Mipango ya mazishi ambayo inatarajiwa kuvuta maelfu ya watu na
mamia ya viongozi wa kimataifa inatarajiwa kutangazwa punde.
Mandela akiwa na Walter Sisulu gerezeni Kisiwa cha Robben.
Bw.
Mandela (95) alikuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya Kusini kufuatia
kutokomezwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi uliofanywa na Makaburu kwa
karibu miaka 400 ambapo watu weupe walijipa haki ya kuwatawala na
kuwabagua watu weusi. Kabla ya kuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee
Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27 jela ambako pamoja na kazi ngumu
aliendelea kuongoza kundi la wapigania haki wengine kudai usawa, utu,
na umoja wa Waafrika ya Kusini. Mandela alikuwa ni mfungwa maarufu zaidi
wa kisiasa duniani ambapo harakati za kutaka afunguliwe zilipiganwa na
wanaharakati sehemu mbalimbali duniani licha ya upinzani wa Serikali ya
Afrika ya Kusini na Baadhi ya Nchi za Kimagharibi ambazo zilimuona
Mandela kama Ghaidi na mchochezi.
Maisha yake ya awali.
Mzee
Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 katika kijiji cha Mvezo mji mdogo wa
Umtatu Jimbo la Cape. Akiwa ni mmoja wa watoto wa Mzee Gadla Henry
Mphakanyiswa Nelson Mandela alikulia kwa mamake – mke wa tatu wa Mzee
Gadla – katika kijiji cha Qunu ambako pamoja na shughuli nyingine za
nyumbani alikuwa mvulana mchunga ng’ombe.
Baadaye
alianza masomo ya shule ya msingi na baadaye Sekondari ambapo aliamini
kuwa alikuwa anaandaliwa kwa ajili ya utumishi katika nyumba ya Chifu wa
Kabila lake la Xhosa kama mshauri. Hata hivyo baada ya kurudi nyumbani
kutoka masomoni mwaka 1940 alikuta kuwa Chifu Jongintaba ameandaa ndoa
Nelson Mandela pamoja mtoto wa kiume wa Chifu huyo aitwaye Justice
walitoroka nyumbani na kwenda kwenye Jiji la Johannesburg. Alifanya kazi
kama mlinzi katika Kampuni ya Madini ya Crown lakini alifukuzwa kazi na
msimamizi wa pale baada ya kugunduliwa kuwa alikuwa ametoroka kwao.
Mandela akiwa amevaa mavazi ya kabila lake la Xhosa; alitoka katika familia ya kichifu.
Kuingia Katika Siasa.
Alipokuwa
akiishi kwa muda na mmoja wa binamu zake Nelson Mandela alitambulishwa
kwa mwanaharakati wa chama cha ANC Bw. Walter Sisulu ambaye baadaye
walifungwa pamoja – Sisulu akitumikia miaka 25 jela. Walter Sisulu
alimtafutia kazi ya ukarani katika kampuni ya Wanasheria ya Witkin,
Sidelsky and Edelman. Akiwa hapo alifanya masomo ya elimu kwa njia ya
Posta ambapo alikuwa anatafuta shahada yake ya kwanza. Mwaka 1943
alihitimu masomo yake ya sheria na kuanza kazi kama Mwanasheria badala
ya kurudi kijijini kutumika kwa Chifu.
Akiwa
ameanza kazi kama Mwanasheria Mandela aliendelea kuwa chini ya uangalizi
wa Walter Sisulu ambaye alikuwa anaendeleza harakati za kudai haki za
weusi. Akikutana mara kwa mara na wanaharakati wengine nyumbani kwa
Sisulu Mandela alikutana tena na rafiki yake Oliver Tambo. Ilikuwa ni
katika mikutano hiyo alikutana na mwanamama Evelyn Mase ambaye walianza
uhusiano wa mapenzi na baadaye kufunga ndoa yake ya kwanza Oktoba ,
1944. Walijaliwa watoto wawili wa kiume na wa kike; wa kiume Madiba
“Thembi” Thembikile alizaliwa Februari 1946 na wa kike Makaziwe
alizaliwa mwaka uliofuatia lakini alifariki miezi tisa baadaye baada ya
kupata maambukizi ya ugonjwa uti wa mgongo.
Mandela na mtoto wake wa kwanza wa kiume Themi.
Baada ya
uchaguzi wa 1948 ambapo watu weupe peke yao walishirikia vyama vya
Herenigle Nacionale Party na Afrikaner Party viliungana na kuunda chama
cha National Party ambacho kilikuwa na sera ya wazi ya ubaguzi na
kikapisha na kupanua ukali wa sera ya ubaguzi kupitia sheria mbalimbali
za ubaguzi wa rangi. Serikali ya Kikaburu ikaja na mojawapo ya Sheria
kali kabisa za kupambana na wanaharakati ambayo inajulikana kama
Ukandamizaji wa Ukomunisti ya 1950. Sheria hii ilikuwa inashughulikia
karibu mambo yote yanayohusiana na kuipinga serikali na ikiwahusu watu
wote.
Migongano kati ya ANC na Serikali ya Kikaburu ilianza kupamba moto.
Mwaka
1952 Nelson Mandela alikamatwa na utawala wa Makaburu kwa kile
kilichodaiwa kujihusisha na vitendo vya Kikomunisti chini ya ile sheria
iliyopitishwa miaka michache nyume. Alihukumiwa miezi tisa jela na “kazi
ngumu” lakini utekelezaji wa hukumu hiyo ulisitishwa kwa miaka miwili.
Lakini mwezi Disemba mwaka huo huo Mandela alipigwa marufuku kuzungumza
na zaidi ya mtu mmoja kwa miezi sita. Akiwa kiongozi wa ANC hii
ilimaanisha kuwa asingeweza kufanya mikutano na wanachama wake. Mwaka
1953 Mandela na rafiki yake Oliver Tambo walifungua kampuni yao ya
Wanasheria katika Jiji la Johannesburg na kuifanya kuwa kampuni ya
kwanza ya Wanasheria Weusi katika Afrika ya Kusini. Walijishughulisha na
malalamiko mbalimbali ya wananchi hasa yanayohusiana na ukatili wa
kisiasa.
Hata
hivyo serikali ikitumia sheria nyingine ikalazimisha kufungwa kwa ofisi
hiyo iliyokuwa na wateja wengi na kuihamisha sehemu nyingine ambapo
ilikuwa ni vigumu kwa wateja kuifikia. Mwaka 1955 Mandela na wenzake
walishirikiana kuandaa kongamano kubwa la watu wa Afrika Kusini ambao
wanaamini katika taifa moja la watu wamoja japo wanatoka katika makabila
na rangi mbalimbali.
Katika
kongamano hili kulisainiwa kile kinachoaminika kama mojawapo ya nyaraka
muhimu kabisa za kutetea usawa na utu wa watu wote ambayo ilijulikana
kama Freedom Charter. Kufananisha hii ni sawasawa na Azimio la Uhuru la
Marekani au ile nyaraka ya Waingereza ya Magna Carta. Kwa Tanzania
tunaweza kufananisha kabisa na Azimio la Arusha. Freedom Charter
ilitengeneza ramani ya kujenga taifa la watu walio huru na sawa katika
Afrika Kusini.
Nelson Mandela na Oliver Tambo – wanasheria
Marafiki wawili – miaka mingi toka Kisiwa cha Robben
Hata
hivyo kwa upande wa familia ndoa yake kwa Evelyn ilianza kuwa matatani.
Kulikuwa na tuhuma za kukosa uaminifu ambapo alidaiwa kuwa na mahusiano
ya mapenzi na baadhi ya kina dada wa ANC. Evelyn alijaribu watengane
lakini pamoja na jitihahada mbalimbali za kupatana Nelson Mandela
aliamua kupeana talaka na mke wake wa kwanza mwezi Machi 1958. Walikuwa
wamejaliwa mtoto mwingine wa kike. Wakati huo wa mchakato wa talaka
Nelson Mandela alikuwa ameanza mahusiano na Winnie Madikizela mmoja wa
wafanyakazi wa mambo ya kijamii. Walifunga ndoa Mwezi Juni 1958.
No comments :
Post a Comment