Msanii Mrisho Mpoto akielezea kupitia mashairi
Mama Zaida Mgalla akitoa ufafanuzi kwa ripota wa Uwezo TV Bi. Melania Mhagama
Mgeni Rasmi akionyesha ripoti baada ya kuzindua.
Mgeni
Rasmi Salum Mjagila, Mkurugenzi, Elimu ya Watu Wazima MOEVT, akikabidhi
ripoti kwa mwakilishi wa wanafunzi ambae pia ni ripota wa Uwezo TV, Bi.
Fatma Bakari
Rakesh Rajani, John Ulanga, Zaida Mgalla na waalikwa wakifurahia jambo
Wakati ambapo asilimia 100 ya watoto wa Darasa la 3 na kuendelea wanapaswa kuweza kusoma na kufanya hesabu za kiwango fulani, matokeo ya Uwezo yanaonyesha kwamba ni wachache tu ndiyo wanaoweza kufanya hivyo.
Katika Darasa la 3, mmoja kati ya watoto wanne anaweza kusoma Kiswahili kwa kiwango sahihi. Shule za binafsi zinafanya vizuri zaidi kidogo kulinganisha na zile za Serikali, ambapo asilimia 61 ya watoto walio na umri chini ya miaka 9 hawawezi kusoma Kiswahili na kufanya Hesabu za Kuzidisha kulinganisha na asilimia 85 ya wenzao walio katika shule za Serikali.
Matokeo haya
yalitangazwa na Twaweza, inayosimamia Tafiti ya Uwezo, katika ripoti
yake ya tatu ya Tathmini ya Mwaka ya Ujifunzaji. Matokeo haya yamejikita
zaidi kwenye tathmini kubwa kabisa ya mwaka kwa ngazi ya kaya inayopima
stadi za kusoma na kufanya hesabu za msingi za watoto.
Tathmini ilifanyika
nchi nzima mwaka 2012; ikipima watoto 104,568 wenye umri kati ya miaka 7
hadi 16 katika kaya 55,191, katika maeneo (vijiji) 3,752, kwenye
wilaya 126 za Tanzania.
Tathmini ya Uwezo inaonyesha kwamba utendaji uko duni nchini kote. Matokeo muhimu yalikuwa:
Stadi ya kusoma Kiswahili – Matokeo bado ni duni na hayajabadilika sana tangu 2011Mtoto 1 tu kati ya 4 (26%) wa Darasa la 3 anaweza kusoma
hadithi ya ngazi ya Darasa la 2.
Kwa Darasa la 7, mtoto 1 kati ya 4 (24%) bado hakuweza kusoma hadithi ya ngazi ya Darasa la 2.
Stadi ya kusoma Kiingereza – Matokeo yalikuwa mabaya zaidi kuliko katika Kiswahili
Katika Darasa la 3, 1 tu kati ya watoto 10 (13%) aliweza kusoma hadithi ya ngazi ya Darasa la 2. Hata katika Darasa la 7, ni watoto 5 kati ya 10 walioweza kusoma hadithi ya ngazi ya Darasa la 2. Kufanya hesabu –
Matokeo yamepanda zaidi kuliko mwaka 2011 lakini bado ni duni Katika
Darasa la 3, zaidi kidogo ya watoto 4 tu kati ya 10 (44%) walioweza kufanya
Hesabu za kuzidisha.
Kufika Darasa la 7, mtoto 1 tu kati ya 10 (11%) aliweza kufanya Hesabu ya ngazi ya Darasa la 2.
Matokeo haya
yanaonyesha kwamba kundi kubwa kabisa la watoto halipati ujuzi
muhimu katika elimu ya msingi. Hata wanapomaliza elimu ya msingi, watoto
bado wanashindwa kufanya zoezi la ngazi ya Darasa la 2.
Kuna tofauti kubwa nchini: Tathmini ya Uwezo inaonyesha jinsi tofauti ya kimatabaka inavyozidi kukua. Watoto katika maeneo ya mijini wanafanya vizuri zaidi kuliko wenzao wa vijijini katika masuala ya kusoma na kuandika.
Watoto
wanaotoka kwenye kaya zenye kipato cha juu vilevile walionekana kufanya
vema zaidi katika stadi hizi za msingi, sawa sawa na watoto wanaosoma
katika shule za binafsi. Ingawa matokeo ya kujifunza kwa ujumla wake ni
duni, tofauti hizi zinazozidi kukua zinaonyesha kuwa mfumo wa elimu
unawanufaisha zaidi wale wenye hali bora.
Watoto
wote, bila kujali umri, darasa au hadhi ya shule walijaribiwa kwa
kutumia ngazi ya kusoma na kufanya hesabu ya Darasa la 2. Matokeo muhimu
yalikuwa:
Mahali
Katika umri wa miaka 9, ni watoto 3 tu kati ya 10 (32%) wa mijini walio
na ujuzi huo wa msingi, kulinganisha na mtoto 1 tu kati ya 10 (11%) wa
vijijini.
Utajiri
Katika umri wa miaka 9, ni watoto 2 tu kati ya 10 (21%) kutoka katika
kaya tajiri zaidi walio na ujuzi huo wa msingi, kulinganisha na chini ya
mtoto 1 kati ya 10 (6%) kutoka kaya maskini.
Aina
ya Shule Katika umri wa miaka 9, ni zaidi kidogo tu ya mtoto 1 kati ya
10 (15%) katika shule za umma aliyefaulu majaribio hayo wakati ambapo ni
watoto 4 kati ya 10 (39%) kutoka shule binafsi walioweza kufanya hivyo.
“Kuna
habari kuu mbili katika elimu ya Tanzania leo,” alisema Zaida Mgalla,
Mratibu wa Nchi wa Uwezo Tanzania “Kwanza, watoto walio wengi
hawajifunzi kitu. Pili, sisi ni jamii ya matabaka mawili – lile lenye
utajiri zaidi au la mjini au linaloweza kumudu gharama za shule za
binafsi na hivyo watoto wao kufanya vizuri zaidi shuleni kuliko watoto
wengine.
Linapokuja
suala la elimu, Tanzania si nchi moja.” Tathmini ya Uwezo ya mwaka 2012
iliendeshwa na wananchi waliojitolea 7,560, ambao walisimamiwa na
washirika katika wilaya 126 nchini (Wilaya za Mtwara hazikujumuishwa kwa
sababu viongozi wa Mkoa hawakuruhusu utafiti
kuendeshwa mwaka 2012). Lengo lilikuwa ni kuwashirikisha wananchi
katika mchakato wa kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuhakikisha watoto
wetu wanajifunza.
Mkuu
wa Twaweza, Rakesh Rajani, alisema “Kuinua ubora wa elimu ni jukumu la
msingi la Serikali; hata hivyo jukumu hili inatuhusu sote. Hatua
zichukuliwe katika ngazi zote, na kila mmoja – kuanzia wazazi hadi
watunga sera, kuanzia walimu hadi maofisa wa wilaya – kila mmoja ana
mchango wa kipekee katika kuhakikisha watoto wetu wanajifunza.”
No comments :
Post a Comment