NA BASHIR NKOROMO
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kikao chake
kilichofanyika jana mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya
Kikwete imeibuka na masuala mazito kadhaa, ambayo leo, Katibu wa NEC,
Itikadi na Uenezi Nape Nnauye (pichani) ameyaeleza wakati akizungumza na
waandishi wa Habari, Katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Lumumba jijini Dar es Salaam.
Moja ya mambo ambayo Nape amezungumzia, ni kuhusu Kamati Kuu hiyo
kuwahoji Mawaziri saba, kujibu kero au mambo kadhaa ambayo yaliibuliwa
wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana iliyomalizika
hivi karibuni katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Mbeya na Njombe.
Nape alisema, Kamati Kuu iliwahoji mmoja baada ya mwingine,
kuanzia saa tano asubuhi hadi jioni, baada ya kila mmoja kufika akiwa
ameandaa majibu ya tuhuma au hoja alizokuwa ametakiwa kujibu mbele ya
Kamati Kuu hiyo.
"Kwa kuwa mawaziri hao tulikuwa tumeshawapelekea hoja zinazowahusu
ambazo tulizipisha kwa kiranja wao Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wengi
wao walifika wakiwa na mafaili yenye majibu, ambapo waliingia na
kujieleza mmoja baada ya mwingine, na baada ya maelezo ya kila mmoja
wajumbe walitoa mapendekezo kwa Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete",
alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema, si vema kueleza kwenye vyombo vya habari
kuhusu mapendekezo ambayo Kamati Kuu ilimshauri Mwenyekiti kuchukua,
akisema kufanya hivyo itakuwa sawa na kumshinikiza kiongozi huyo
kutekeleza mapendekezo yao kwa lazima na hivyo kuharibu maana nzima ya
ushauri.
"Sisi tulichofanya ni kumpa mapendekezo, naye kwa mujibu na namna
atakavyoona inafaa, atachukua hatua, ambavyo si lazima kumfukuza Waziri
Kama wengi wanavyotaka iwe, bali anaweza kuchukua hatua yoyote ili mradi
yeye mwenyewe kwa mamlaka aliyo nayo ataona ina manufaa yatakayotoa
majibu ya kero zilizosaababisha kila mmoja wa mawaziri hao kuitwa mbele
ya Kamati Kuu", alisema Nape.
No comments :
Post a Comment