Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
mchezaji wa zamani wa timu ya Simba na Taifa Stars, Gebo Peter
kilichotokea usiku wa kuamkia leo (Juni 6 mwaka huu) katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Gebo
aliyezaliwa mwaka 1961, pia aliwahi kuchezea timu za Sigara ya Dar es
Salaam, CDA ya Dodoma na kombaini ya Mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima
United). Hadi mauti yanamkuta alikuwa akijishughulisha na biashara,
kubwa ikiwa ya vifaa vya michezo.
Msiba
huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu nchini kwani, Gebo enzi
za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa mchezaji na baadaye kiongozi
katika timu ya Manyema ya jijini Dar es Salaam.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Gebo Peter, klabu ya Manyema na
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa
na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Msiba upo nyumbani kwao Vingunguti karibu na Kanisa Katoliki ambapo taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na familia.
Marehemu
ambaye ameacha mjane na watoto watatu anatarajiwa kuzikwa kesho (Juni 7
mwaka huu) nyumbani kwao Kigurunyembe, mjini Morogoro.
Bwana alitoa, na Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina
No comments :
Post a Comment