Add caption
TIMU ya Mpira wa miguu ya Mbeya City Fc
inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeanza kujihakikishia kufanya
vizuri zaidi kwa msimu ujao baada ya kupata rasmi mdhamini.
Kampuni ya Bin Slum Company Limited yenye
makao makuu jijini Dar Es Salaam ndiye kampuni ya kwanza kukubali kuwa mdhamini
wa timu hiyo kwa miaka miwili kwa kitita cha shilingi Milioni 360.
Utilianaji sahihi wa mkataba umefanyika leo katika Ukumbi wa
Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Mbeya baina ya Uongozi wa Kampuni hiyo na
Halmashauri ya Jiji la Mbeya mbele ya vyombo mbali mbali vya habari.
Akizungumza na vyombo vya habari katika
hafla hiyo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mohamed Binslum, alisema kampuni yake
imefikia makubaliano hayobaada ya kuridhika na uongozi wa Mbeya city namna
ulivyojipanga katika kuendesha timu.
Binslum alisema pia kampuni yake
imeridhika namna timu hiyo ilivyopata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wa
Jiji la Mbeya pamoja na mikoa ya Nyanda za juu kusini.
Aliongeza kuwa katika mkataba huo wenye
thamani ya Shilingi Milioni 360 kampuni hiyo itakuwa ikitangaza bidhaa zake ambazo ni RB
Battery katika Jezi za Timu ya Mbeya city na nyuma ya jezi chini ya namba
itaandikwa jina la kampuni la Binslum Tyre Company.
Mkurugenzi huyo alisema kuingia Mkataba
na Mbeya city ni fursa pekee ya Kampuni kutangaza bidhaa zake za Betri aina ya
RB ambazo zina soko kubwa Mkoani Mbeya pamoja na bidhaa zingine ambazo ni
matairi aina ya Double star na vee rubber.
Kwa upande wake Katibu wa Timu ya Mbeya
city, Emmanuel Kimbe, mbali na kuishukuru kampuni hiyo kwa kukubali kuwa
mdhamini wa Mbeya city pia alimuahidi kutekeleza kile mdhamini anachotarajiwa
kukipata kwenye timu hiyo.
Alisema Mbeya city inadhumuni la
kutangaza bidhaa za Bin Slum kupitia jezi za mechi za ndani, Nje na mazeozi ikiwa ni pamoja na timu kuendelea
kufanya vizuri.
Aliongeza kuwa mbali na kupata mdhamini
lakini wamiliki wa timu pia wataendelea kufanya majukumu yao kwa ajili ya timu
kama kawaida na kuongeza kuwa mkataba huo unaanza Juni Mosi Mwaka huu hadi Mei
31, 2016.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro,alisema Halmashauri imepata faraja kubwa
kupata mdhamini kutokana na Halmashauri kutokuwa na fedha za kutosha kuweza
kuendesha timu.
Alisema kuendesha timu kunahitaji kuwa na
uchumi mkubwa ambao Halmashauri haina hivyo kupitia mdhamini huyo timu ya Mbeya
city itafanya vizuri zaidi katika msimu ujao.
Mwisho.
Na Mbeya yetu |
No comments :
Post a Comment