Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad
akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata
ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro. (Picha na Salmin Said,
OMKR)
MOROGORO, T anzania
Chama Cha Wananchi CUF kimesema kuwa kinakusudia
kujenga uchumi imara utakaoweza kumnufaisha kila Mtanzania popote alipo bila ya
ubaguzi wa aina yoyote.
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad
ameeleza hayo wakati akifunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kwa chama
hicho katika kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Amesema Watanzania bado hawajanufaika ipasavyo
kutokana na rasimali zake zikiwemo ardhi, madini na wataalamu, hali inayotokana
na mfumo wa uongozi usiozingatia mgawano wa rasilimali za nchi kwa maslahi ya
wananchi.
“Mimi nashangaa sana, kwa nini serikali ya Tanzania
inashindwa kumtumia Prof. Lipumba, wakati nchi nyengine za Afrika Mashariki na
jumuiya za kimataifa zinamtumia vizuri kukuza uchumi wa nchi na taasisi hizo”,
alihoji Maalim Seif.
Amefahamisha kuwa CUF ni chama chenye sera za
kumkomboa mtanzania, na kuwaomba wananchi wa mkoa huo kukiunga mkono ili kuleta
mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi katika eneo hilo na mikoa mengine ya
Tanzania.
“Wananchi tunahitaji kuleta mabadiliko ya msingi
katika nchi yetu, tatizo tulilonalo sasa ni viongozi wasiokuwa na dira ya
mabadiliko”, alifahamisha.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa haki za binadamu,
uenezi, mawasiliano na umma wa Chama hicho Bw. Abdul Kambaya amesema wananchi
wa kata ya Mtibwa wana kila sababu ya kuleta mabadiliko ya uongozi katika eneo
hilo kutokana na manufaa madogo wanayoyapata licha ya kuwa na rasilimali zilizowazunguka.
“Sukari kwa mfano, inazalishwa katika kata hii ya
Mtibwa lakini wananchi wa Mtibwa munanunua sukari kwa bei sawa sawa na
wanavyonunua wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, kulikoni”? alihoji Kambaya.
Amefahamisha kuwa wananchi wa eneo hilo pia wamekuwa
wakikosa msingi bora wa elimu kutokana na ukosefu wa walimu unaotokana na mfumo
mzima wa elimu na uongozi unaolenga kuwanufaisha zaidi watoto wa viongozi.
“Sijui kuwa yupo mtoto wa Waziri, Katibu Mkuu au
Mkurugenzi anaesoma katika skuli hii, ndio maana hamuendelei na munaishia
darasa la saba, mutapataje ajira kwa elimu ya darasa la saba wakati huu, wao
watoto wao wanawasomesha katika ‘International Schools’ hadi kumaliza madigrii
yote, nyinyi mmelala tu munajisahau baada ya kufurahishwa kwa nyimbo za
wasanii”, alifahamisha.
Kabla ya mkutano huo wa kufunga kampeni za udiwani,
Maalim Seif alizungumza na wazee wa CUF wa Mkoa wa Morogoro, na kuwashukuru kwa
kuendelea kukiunga mkono chama hicho.
“Nashkuru kuwa kwa muda wote huo hamkuyumba na
hamkubali kuyumbishwa katika kutetea chama chenu, nakushkuruni sana kwa msimamo
wenu huo”, aliwapongeza.
Nao wazee hao ambao kwa kiasi kikubwa
wanajishughulisha na kazi za kilimo, wameelezea masikitiko yao ya kuhujumiwa
kwa kilimo chao na wafugaji, jambo ambalo limekuwa likizorotesha maendeleo yao.
Wamemshukuru Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye pia ni
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kwa kufika katika eneo hilo na kubadilishana
mawazo juu ya changamoto mbali mbali zinazowakabili, na kuelezea kufarajika
kwao kutokana na ujio wake.
No comments :
Post a Comment