Na Onesmo Ngowi
Masumbiwi
au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa,
mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni
kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini
kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha
nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana
kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa
endelea………………………………….!
MATUMIZI YA SHERIA MPYA ZA NGUMI
Ni
katika mwaka 1866 wakati ambapo mtawala wa Queensbury (Marguees of
Queensbury) huko Uingereza alisaidia kutunga sheria mpya zilizotumika
kuuendesha mchezo wa ngumi sheria ambazo kwa heshima zilipewa jina lake.
Sheria hizi ziliweka bayana mambo yafuatayo:
Uzito
wa kila bondia ulianzia Fly ambao ni chini ya kilo 50, bantam kilo 54,
featherweight kilo 57, lightweight kilo 60, welterweight kilo 67,
middleweight kilo 75, light heavy kilo 80 na hevyweight uzito ambao
haukuwa na kikomo.
Sheria za ulingoni: zilipunguza
muda uliotumika kwenye raundi za mpambano wa ngumi kuwa dakika 3, na
pia ziliweka kikomo kwa mabondia kuangushana chini kama wacheza mieleka.
Zilifanya pia matumizi ya gloves kuwa ya lazima. Uzito wa glovu nao
ulianzia oz 8, 9, 10, 12 na 15.
Pamoja
na ukweli kwamba sheria hizi mpya za hazikuweza kuzuia kwa mara moja
kupigana kwa kutumia mikono mitupu (bare-knuckle). Ushindi wa bondia
maarufu wa Kingereza James J. Corbet dhidi ya bingwa maarufu
aliyejulikana kwa kucheza kwa mikono mitupu John L. Sullivan mwaka 1892
ndipo matumizi ya gloves yalipoanza kutumika rasmi katika mapambano yote
ya ngumi.
Katikati
ya karne ya 20 kuelekea kwenye karne ya 21 sheria mpya za ngumi
zilitungwa baada ya kuanzishwa kwa mashirikisho mbalimbali ya ngumi
ambayo kila moja lilikuja na sheria zake. Kwa uchache sheria hizi
zilipunguza raundi za ngumi mpaka kufikia 15 kwa ubingwa wa ngumi na
kuweka sheria kali za sehemu ambazo bondia anaweza kumpiga mwingine.
Aidha
sheria hizi ziliweka kikomo katika uzito mbalimbali ambapo kulianzishwa
uzito kama light fly, fly, super fly, light welter, junior middle,
super middle n.k. Vile vile sheria hizi mpya zilizuia matumizi ya madawa
mbalimbali ya kuongeza nguvu kwa mabondia.
Katika
mashindano makubwa ya kimataifa hususan Olimpiki wakati wa ngumi za
ridhaa sheria za matumizi ya madawa ya kuongeza ngumi ziliwekewa
kipaumbele. (Wakati huu madawa mengi ya kuongeza nguvu yamepigwa
marufuku karibu katika michezo yote).
Aidha
mabondia mbalimbali ambao waligombea mikanda ya ubingwa walitakiwa
walingame uzito na aliyezidi ilibidi apewe muda maalum wa kuupungunza
hadi afikie uzito wa mwenzie.
Ni
mwishoni mwa karne ya 20 ndipo mashindano makubwa ya utitiri wa
mashirikisho ya ngumi hususan ngumi za kulipwa yalipoanzishwa kwa fujo
za aina yake.
Mwanzoni
kulikuwepo na shirikisho moja tu nalo lilikuwa Chama cha Ngumi duniani
(WBA). Baada ya muda wa miongo kadhaa Baraza la Ngumi Duniani (WBC) nalo
lilianzishwa. Mwanzoni mwa miaka ya 80 Shirikisho la Ngumi la Kimataifa
(IBF) nalo lilianzishwa.
Sababu
kubwa ambazo zinatajwa na watu mbalimbali za kuwepo kwa utitiri wa
mashirikisho haya ni ubinafsi. Lakini ukiangalia kwa makini kuanzishwa
kwa mashirikisho haya kumeweza kwa kiasi kikubwa kuwapa nafasi mabondia
wengi kujulikana kimataifa.
Hebu
fikiria kuwa katika nafasi ya ubingwa wa shirikiso moja kuna nafasi 17
tu za ubingwa. Kwa maana nyingine mabondia 17 tu ndio wanatakiwa
wajulikane kuwa ni mabingwa wa dunia kwa wakati mmoja.
Idadi
kamili ya mabondia walioko dunia nzima haijulikani lakini inaweza
kufikia malaki kama sio mamilioni kadhaa. Itakuwa vigumu sana kwa
mabondia wote kuweza kufikia ubingwa wa dunia katika maisha yao kama
kungekuwepo na shirikisho moja tu.
Japokuwa
kuna hisia kuwa mashirikisho mengine yamezidiwa umaarufu na mengine
lakini kunasaidia kuwapa nafasi nzuri mabondia wengi kujulikana duniani.
Kwa sasa inakadiriwa kuweko kwa mashirikisho kama 15 na ukizidisha kwa
17 utaona tayari mabondia wengi zaidi wanaweza kuwa mabingwa wa dunia
kwa wakati mmoja. Japokuwa bingwa mmoja wa dunia anaweza kujulikana kwa
zaidi ya shirikisho moja.
SHERIA ZA BAADHI YA MASHIRIKISHO YA NGUMI
Mashirikisho mengi ya ngumi yanatumia sheria zinazofanana. Yote yanatumia sheria za “Marguees of Qunensbury” yaani
mabondia wapigane wakiwa wamevaa glovu mikononi zenye uzito unaofanana.
Wawe na uzito sawa na ngumi zipigwe kuanzia juu ya mkanda.
Ikumbukwe
kuwa mengi ya mashirikisho haya yalianzishwa miaka ya karibuni. Kabla
ya shirikisho hata moja la ngumi kuanzishwa ngumi zilikuwa zinatawaliwa
(zinaendeshwa) na kamisheni za mitaa, manispaa na nchi mbalimbali. Hata
wakati mabondia wa zamani wanatwa ubingwa wa dunia kwao hakukuwa na njia
mbadala ya kuwakutanisha na mabondia wengi waliokuwa kwenye viwango
vimoja na wanotoka katika nchi mbalimbali.
Ikumbukwe
pia kwamba neno ubingwa wa ngumi linamaanisha ushindi wa tuzo katika
kiwango chako. Kama unawashinda mabondia karibu wote walio kwenye
kiwango chako unakuwa bingwa wa kiwango hicho. Viwango huwekwa na
mashirkisho yanayosimamia ngumi.
Kwa
mfano mabondia wanaowekwa kwenye viwango fulani vya ngumi wanatakiwa
wawe wamecheza mapambano kadhaa yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa.
Shirikisho
la Ngumu la Kimataifa (IBF) linataka walio kwenye viwangio vyake wawe
wameshindana na mabondia wenye hadhi ya kimataifa. Viwango vya IBF
vinaanzia 1-15 kila uzito. Bondia
anayeingizwa kwenye viwango vya IBF ni lazima awe amecheza mapambano
zaidi ya 15 yenye hadhi ya kimataifa ya kushinda asilimia 75 ya
mapambano yote.
Yapo
mashirikisho mengine yenye utaratibu tofauti na wa IBF na ambayo
masharti ya kuingizwa kwenye viwango vyake sio magumu sana. Pengine ndio
maana mashirikisho ya IBF, WBA, WBC na WBO yanaheshimika zaidia duniani
kwa kuwa masharti ya kuwekwa kwenye viwango vyake na kucheza ubingwa
wake ni magumu zaidi.
Kwa
ajili ya sheria kuwa ngumu mashirikisho haya yana makubaliano ya
kuwaruhusu mabondia kucheza ubingwa unaotambuliwa na mashirikisho yote
manne kwa pamoja (unification titles). Yaani bondia anaweza kugombania
ubingwa mmoja unaotambuliwa na IBF, WBA, WBU na WBO na kuvaa mikanda
minne. Mabingwa hawa wanajulikana kama undisputed champions (mabingwa
wasiopingika)
Sina
maana kwamba ubingwa wa mashirikisho mengine hauna maana bali
yamezidiana kwa umaarufu na heshina tu. Bingwa wa dunia ni bingwa kwa
wapenzi wake na wapinzani wake.
Wako
mabingwa wa mashirikisho mengine kama IBA, IBC, WBF, WPBF ambao
wamekuja baadaye kuwa mabingwa wa sasa wa WBC, WBA, IBF na WBO. Mfano
mmoja ni bingwa wa sasa wa WBC Vitali Klitschko toka Ukraine ambaye kwa
muda mrefu alikuwa bingwa wa dunia wa WBO. Iaendelea………………………….!
Mwandishi
wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania
(TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF),
Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati,
Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi
la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com
No comments :
Post a Comment