UONGOZI
wa klabu ya Yanga umeanzisha mchakato wa kupiga kura kwa wanachama wake kuamua
hatma ya klabu yao kuwa kampuni au kubaki kama klabu ya soka ya kawaida.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu wa klabu hiyo, Lawrance Mwalusako
ilisema kuwa wanachama hai wote watakuwa na haki ya kupiga kura na kutoa
maamuzi yao.
Mwalusako
alisema kuwa maamuzi hayo ni utekelezaji tu wa kile walichoamua katika mkutano
wa Wanachama uliofanyika 16 Januari, 2013 ambapo Mwenyekiti kwa niaba ya Kamati
ya Utendaji aliwapa Wanachama wafikirie mapendekezo ya Yanga kuwa Kampuni ama
kutokuwa Kampuni kisha kuyawasilisha kwa katibu mkuu wa Yanga.
Katibu
huyo alisema kuwa anaamini kuwa wanachama wamefikiria vya kutosha hivyo kuanzia
leo 16 Oktoba, 2013 mpaka 10 Novemba, 2013, kutakuwa na sanduku moja (1) klabuni
kwa ajili ya kukusanya kura za maoni ambapo wanachama wanaotaka Yanga kuwa kampuni
watapiga kura ya (NDIYO) au wasiopenda wataandika (HAPANA)
Alisema kila
mwanachama hai atakuwa na uhuru wa kupiga kura na atalazimika kuja na Kadi yake
ambapo itamzuia kupiga kura mara mbili au zaidi. Zoezi hili ni muhimu kwa ajili
ya maendeleo ya YANGA.
No comments :
Post a Comment