MBUNGE wa Bukoba vijijini, Jasson Rweikiza, ameitaka
serikali kuangalia upya utaratibu wa utoaji vibali kwa walimu kutoka
Jumuia ya Afrika Mashariki.
Rweikiza alitoa ombi hilo juzi, kwenye mahafal ya tatu ya
kidato cha nne, shule ya sekondari Brilliant, iliyopo Mbezi kwa Msuguri
jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Alisema Tanzania ina upungufu wa walimu zaidi ya 130,000,
lakini shule binafsi haziwezi kuagiza kutokana na urasimu na gharama
kubwa za kibali cha kazi.
"Nchi ina uhaba wa walimu, lakini wenzetu Kenya na Uganda
wana idadi kubwa ya walimu kuliko mahitaji, sasa unapoagiza mwalimu
kutoka nchi hizo, kuna urasimu mkubwa wa kupata kibali, na kikitoka hiyo
gharama yake, utajuta," aliongeza Rweikiza ambaye ni mmiliki wa shule
hiyo.
Alisema pamoja na mambo mengi kuchangia matokeo mabaya kwa
wanafunzi, lakini ukosefu wa walimu ni sababu kubwa zaidi inayochangia
matokeo hayo mabovu.
Aliitaka serikali kuruhusu walimu kutoka nchi hizo kuja kufundisha na nchi itakapojitosheleza basi waondoke.
Aliitaka serikali kuruhusu walimu kutoka nchi hizo kuja kufundisha na nchi itakapojitosheleza basi waondoke.
Naye mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes ambaye alikuwa
ameambatana na Ngeleja, alisema watalipigia kelele suala hilo pindi
wakifika bungeni.
"Wenye mapenzi mema na taifa, tusukume jambo hili lifanikiwe ili kunusuru elimu,"alisema.
Ngeleja akijibu hoja hizo kwa majumuisho alisema watapigia debe uingiliano huru wa kazi kwa nchi za Afrika Mashariki
Aliahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kumpa
nguvu Rweikiza katika kukamilisha ujenzi wa shule, kwani uwekezaji
kwenye elimu haumsaidii yeye na familia yake tu bali taifa zima.
Ngeleja aliahidi pia kwenda kuzungumza na Waziri wa Ujenzi,
ili kushughulikia tatizo la ubovu wa barabara zinazoingia shuleni hapo
na nyingine zaidi ya sita zinazozunguka eneo hilo.
No comments :
Post a Comment