Kwa niaba ya Wana-Iringa na hususan wadau wa habari wa mkoani Iringa,
Mtandao wa KwanzaJamii.com na Mjengwablog. com unachukua fursa hii
kuwakaribisha mkoani kwetu Iringa, wahariri wanachama wa Jukwaa la
Wahariri hapa nchini.
Ni heshima kubwa kwetu Wana-Iringa kwa Jukwaa la Wahariri kuichagua Iringa kama mahali pa kufanyia Mkutano wao Mkuu wa Mwaka.
Ni faraja pia, tukikumbuka tukio la kuawa kwa ndugu yetu na
mwanahabari mwenzetu Daud Mwangosi mwaka mmoja uliopita. Tukikumbuka pia
tukio la miezi ya karibuni la kujeruhiwa vibaya kwa mwanahabari na
mhariri wa miaka mingi hapa nchini, Absalom Kibanda.
Ni jambo la kutia matumaini pia, kuwa moja ya ajenda za Mkutano huo
wa Wahariri unaoanza leo Ijumaa na kumalizika kesho Jumamosi ni kujadili
masuala ya Usalama wa Wanahabari.
Ni matumaini yetu, kuwa Wahariri kupitia Mkutano wao huu wa Iringa ,
na wakiwa Iringa yenye hali ya hewa nzuri, Iringa yenye amani, utulivu
na isiyo na hata foleni za barabarani.
Naam, wakiwa mbali sana na news rooms zao, Wahariri hao watapata
fursa ya kujadiliana kwa kina na hatimaye kutoka na ' Azimio La Iringa'
lenye maslahi kwa tasnia ya habari nchini na jamii kwa ujumla.
Na huko mitaani Iringa wahariri muwachangie Wana-Iringa kwa kununua
bidhaa zinazotengenezwa Iringa. Msisahau pia kula vyakula vyetu vya
Iringa ikiwamo na vinywaji pia.
Si mnajua, Iringa tuna maji ya chemchem kama vile Maji Afrika, ya
Mufindi, Image na yale yanayotirika kutoka kwenye miti...! Tuna pia
bidhaa bora zitokanazo na maziwa ya ng'ombe wafugwao hapa Iringa. Hii ni
pamoja na jibini na maziwa bora na maarufu nchini yenye chapa ya 'Asas
Milk'.
Na kwenye mechi yenu ya kesho dhidi ya wanahabari wa Iringa matokeo
hayahitaji utabiri wa Sheikh Yahya. Kwa vile kuna ng'ombe anashindaniwa,
basi, ndugu zangu Wahariri mtambue, kuwa, kwa Mnyalukolo, kwenye
kugombania nyama, hakubali matokeo mengine isipokuwa ushindi tu..!
KwanzaJamii.com na Mjengwablog inawatakia ukazi mwema mkiwa Iringa.
Maggid Mjengwa.
Mwenyekiti Mtendaji.
IkoloMedia.
Iringa.
0754 678 252
No comments :
Post a Comment