Baadhi ya Wachezaji wa Pool kutoa Vyuo Mbali mbali wakicheza mchezo huo ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa Mashindano hayo.
Kampuni
ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager leo imetangaza
rasmi kudhamini kwa mara nyingine tena mashindano ya mchezo wa Pool
Table kwa vyuo vya elimu ya juu hapa Tanzania. Mashindano haya
yajulikanayo kama “Safari Lager Higher Learning Pool Championships”
yanafanyika kwa mwaka wa tatu sasa, Safari Lager imekuwa wadhamini wakuu
wa mashindano haya kwa miaka yote hii mitatu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo meneja wa Safari
Lager,Oscar Shelukindo alisema nia hasa ya kudhamini mashindano haya ni
kuwapa wanafunzi burudani baada ya ratiba ngumu za masomo ili waweze
kupumzisha akili warudi wakiwa na ari mpya. Mapumziko husaidia akili
kufanya kazi kwa haraka na kuwa na ubunifu zaidi.
Shelukindo
aliendelea kusema “Mbali na kupumzisha akili, michezo husaidia
kuwakutanisha watu mbalimbali, kujenga afya bora na katika mazingira
yetu ya sasa mchezo wa Pool umekua zaidi na unaweza kuwa kama fani
nyingine zinazomuingizia mchezaji pesa”. Safari Lager imekuwa wadhamini
wa mchezo wa Pool toka mwaka 2008, imedhamini mashindano ya ndani na ya
nje ya nchi pia. Imedhamini timu ya Taifa ya mchezo wa Pool kushiriki
mashindano ya dunia ya mchezo wa Pool nchini Ufaransa mwezi wa kumi
mwaka 2010 ambapo timu yetu ilifanya vizuri.
Naye
katibu wa chama cha mchezo wa Pool Tanzania (TAPA),Amos Kafwinga
alisema mashindano haya yanaanzia kwa vyuo kushindana katika ngazi ya
mkoa na baadae mikoa yote itashindana katika ngazi ya taifa ili kupata
mshindi wa jumla kwa vyuo vyote.
Mashindano
ya mwaka huu yanatarajiwa kuanza rasmi kutimua vumbi katika mkoa wa
Morogoro Jumamosi ijayo tarehe 12 May 2012. Mashindano ya mwaka huu
yatahusisha wanafunzi wa vyuo vilivyo katika mikoa ya Morogoro, Dodoma,
Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Dar Es Salaam. Mashindano
ya taifa mwaka huu yatafanyika katika mkoa wa Iringa mwanzoni mwa mwezi
wa sita.
Mwaka
jana chuo cha Usimamizi Wa Fedha (IFM) kiliibuka na ushindi katika
mashindano ya kitaifa yaliyofanyika mkoani Dodoma, walijipatia kikombe
na jumla ya shilingi milioni mbili na laki tano. Akizungumzia ushindi
huo,Charles Venance ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho na kiongozi wa
timu ya pool ya chuo alisema fedha hizo ziliwasaidia katika mahitaji
mbalimbali ya masomo. Alisema “Tumejiandaa vizuri sana mwaka huu na kwa
hakika ushindi utabaki IFM, vyuo vyote vitakubali kwamba IFM ni moto wa
kuotea mbali kwenye Pool!”.
Akitoa
shukrani kwa Safari Lager kwa niaba ya Chama cha Mchezo wa Pool
Tanzania (TAPA), Mwenyekiti wa chama hicho,Isaac Togocho alisema
“Taswira ya mchezo wa pool hapa nchini imebadilika kwa kiasi kikubwa na
sasa inawavutia vijana wa kaliba mbalimbali kwani si mchezo wa kupotezea
muda tena kama wengi walivyodhania, Pool ni miongoni mwa michezo
inayokua kwa kasi kubwa na kuwapatia kipato wachezaji na vijana kwa
ujumla. Hii yote imetokana na Bia ya Safari Lager kukubali kuudhamini
mchezo wa Pool table. Kwa niaba ya chama tunatoa shukrani nyingi sana na
kuomba Safari Lager iwe nasi ili tuendelee mbele zaidi”.
Shelukindo
alizitaja zawadi za washindi katika ngazi ya mikoa kuwa timu
itakayoshinda itajipatia kitita cha shilingi laki tano, washindi wengine
watajipatia shilingi laki tatu kwa mshindi wa pili, laki mbili na laki
moja kwa mshindi wa nne. Washindi kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja wa
kiume watajipatia shilingi laki moja na nusu kwa bingwa na laki moja kwa
mshindi wa pili.
Wachezaji
wa kike watajipatia laki moja kwa bingwa na shilingi elfu hamsini kwa
mshindi wa pili. Mshindi katika ngazi ya taifa ataibuka na kikombe
pamoja na jumla ya shilingi milioni mbili na nusu taslim (2,500,000),
jumla ya shilingi milioni tisa na laki tano zitatolewa kama zawadi
katika michuano ya ngazi ya taifa.
Shelukindo
alimalizia kwa kutoa shukrani kwa wanywaji wa bia ya Safari Lager na
wachezaji wote wa mchezo wa Pool kwa ujumla, aliwaomba wajinoe kwani
Safari Lager inadhamini tena mashindano ya kitaifa ya mchezo wa pool
ambayo yataanza hivi karibuni.
No comments :
Post a Comment