Na Francis Godwin ,Iringa
KATIBU mkuu mstaafu wa shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Frederick Mwakalebela amekusudia kujenga shule ya Academia ndani ya Manispaa ya Iringa kwa ajili ya kukuza soka ndani ya mkoa wa Iringa.
Mwakalebela ametoa ahadi hiyo leo baada ya kuimwagia vifaa mbali mbali vya michezo timu ya polisi Iringa ,vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5 kama njia ya kuiandaa timu hiyo kuja kucheza ligi kuu Tanzania bara .
Mwakalebela ambaye pia ni kada wa chama cha mapinfuzi (CCM) amekabidhi vifaa hivyo leo kwa mlezi wa timu hiyo ya Polisi Iringa mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi ofisini kwake .
Akikabidhi vifaa hivyo zikiwemo jezi ,mipira na vifaa vingine vya mazoezi kwa wachezaji wa timu hiyo ,Mwakalebela alisema kuwa amelazimika kutoa msaada huo kwa timu ya polisi Iringa kutokana na jitihada mbali mbali ambazo timu hiyo imekuwa ikiendelea kuonyesha na kuwa polisi Iringa ni moja kati ya timu nzuri zilizobaki katika mkoa wa Iringa ambayo inaweza kufanya vema na kuingia katika mashindano ya ligi kuu Tanzania bara.
Hata hivyo alisema msaada huo ameutoa kwa polisi Iringa kupitia kampuni yake Vannedrick (T)Ltd, inayojishughulisha na uuzaji wa vifaa vya michezo na kukuza viwango vya soko kwa wachezaji na kuwa moja kati ya mikakati ya kampuni yake ndani ya mkoa wa Iringa ni kupata eneo la kujenga uwanja wa kuibua vipaji vya wanamichezo ndani ya mkoa .
Kwa upande wake Mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa ,Mwamwindi akishukuru kwa msaada huo alisema kuwa Mwakalebela amekuwa mdau wa kwanza kuonyesha jitihada zake kwa timu hiyo ya Polisi toka jeshi la polisi lilivyoikabidhi timu hiyo kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa.
Hata hivyo aliwataka wafanyabiashara na wadau wengine ndani na nje ya mkoa wa Iringa kujitokeza kuendelea kuisaidia timu hiyo ya polisi Iringa ambayo kwa sasa ipo kambini kwa ajili ya maandalizi ya ligi daraja la kwanza itakayo anza mapema mwezi ujao.
No comments :
Post a Comment