Kaimu Meneja Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Juma Kintu (kulia), akimkabidhi Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui fedha taslimu sh. milioni tatu kwa ajili ya maandalizi ya timu ya riadha itakayoshiriki mashindano ya Afrika 'All Africa Games' Septemba mjini Maputo, Msumbiji. Katikati ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) Makore Mashaga jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Nyakasagani Masenza)
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umetoa sh. milioni sita za kusaidia kambi ya Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
Kaimu Meneja Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Mfuko huo, Juma Kintu, amesema NSSF imetoa fedha hizo ili kusaidia maandalizi ya michezo ya All Africa Games itakayofanyika jijini Maputo, Msumbiji Septemba mwaka huu.
Kintu alimkabidhi sh. milioni tatu Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, na sh. milioni tatu kwa Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui.
Amesema ili timu hizo ziweze kushiriki mashindano hayo vizuri na kupata ushindi, wachezaji wanatakiwa kupata maandalizi mazuri na mazoezi ya pamoja, ndio maana NSSF imekubali kutoa fedha hizo.
Katibu Mkuu wa BFT, Mashaga amesema shirikisho lake limepokea msaada huo kwa faraja na kuahidi kutumia fedha hizo kwa ajili ya maandalizi ya safari ya Msumbiji.
Amesema wachezaji wataweka kambi ya mazoezi mkoani Arusha na kurejea Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kuelekea Msumbiji, ambapo mashindano hayo yataanza Septemba 3 hadi 18, mwaka huu.
Naye, Katibu Katibu Mkuu wa RT, Nyambui Suleiman pamoja na kuishukuru NSSF, ameahidi vijana wake kufanya vizuri katika mashindano hayo na kuiletea Tanzania medali.
No comments :
Post a Comment