Release No. 123
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 25, 2011
FAINALI UHAI CUP YASOGEZWA
Mechi ya fainali ya michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Kombe la Uhai (Uhai Cup) kwa klabu za Ligi Kuu sasa itachezwa kesho (Novemba 26 mwaka huu) saa 3.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Karume.
Awali fainali hiyo kati ya Simba ambayo iliingia hatua hiyo kwa kuitandika Toto Africans mabao 4-1 na Azam iliyofuzu kwa kuizamisha Serengeti Boys (timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17) mabao 3-0 ilikuwa ichezwe leo (Novemba 25 mwaka huu) saa 9.00 kwenye uwanja huo.
Mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi za michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo (Novemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa. Kila siku kwenye michuano ya Chalenji zinachezwa mechi mbili; ya kwanza saa 8.00 mchana na nyingine saa 10.00 jioni.
Michuano ya Kombe la Uhai inadhaminiwa na Kampuni ya S.S. Bakhresa kupitia maji Uhai ambapo bingwa atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000. Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba.
Mchezaji bora sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu sh. 300,000.
VIINGILIO MICHUANO YA KOMBE LA CHALENJI
Viingilio kwa mechi za hatua ya makundi kwa michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo (Novemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam vitakuwa kama ifuatavyo;
Kwa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni zaidi ya 30,000 kiingilio kitakuwa sh. 1,000 wakati viti vya rangi ya chungwa ambavyo ni zaidi ya 10,000 kiingilio kitakuwa sh. 3,000. VIP C na B ambayo jumla ya viti vyake ni 8,000 kiingilio kitakuwa sh. 5,000 wakati VIP A yenye viti 700 kiingilio ni sh. 10,000.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments :
Post a Comment