Na Imani Makongoro, Mwananchi
Nyumbani kwa
bondia Francis ‘SMG’ Cheka hakuishi pilika ambazo zinatokana na kazi ya
chupa za plastiki anayofanya bingwa huyo wa zamani wa dunia wa WBF.
Nje ya
nyumba yake kuna mafurushi kila kona yakiwa na ‘bidhaa’ tofauti ikiwamo
chupa za plastiki, chupa za konyagi, chibuku na plastiki ngumu (ndoo na
madumu) yaliyopasuka.
Cheka anavyookota chupa
“Mimi ndiyo
mwanzilishi wa biashara hii hapa Morogoro, niliianza 2004 baada ya
kuamua kuingia mtaani kuokota na kuziuza mwenyewe, wakati huo kilo moja
niliuza kwa Sh100 na nilikuwa nikizunguka kutwa nzima kutafuta chupa
mtaani,” anasema Cheka.
Anasema wakati anaanza kuokota chupa alikuwa na miaka mitano tangu aingie kwenye ngumi za kulipwa, lakini hakuwa maarufu.
“Nilikuwa
nina uwezo wa kuzunguka na kuokota hadi kilo 100 kwa siku, japo ilikuwa
kazi ngumu, lakini nilipata fedha nikanunua kiwanja maeneo ya Kilimahewa
na kujenga nyumba kwa kazi ya kuokota chupa.
“Pia
niliweza kujiandalia mapambano peke yangu kwa kazi hii, ambayo
yalinijenga na kunipa umaarufu kwenye ngumi, nimejiandalia mapambano
zaidi ya 15 kwa fedha niliyopata kwa kuokota chupa,” anasema Cheka.
Anasema
vijana wengi wa Morogoro walianza kuokota chupa baada ya kuona Cheka
amejenga nyumba kwa kazi hiyo, hivyo hakuwa na hiyana aliwafundisha kazi
hiyo na wengine aliingia nao mtaani kuokota.
“Nilipoanza
kucheza mapambano ya ubingwa wa Afrika nilisimama kuokota chupa
nikawaachia wengine na mimi kuelekeza nguvu zangu kwenye ngumi, kijiwe
changu nikamweka mtu wa kufanya hiyo kazi na nikawa na nanunua kwa watu
wengine kisha mimi nauza tena.
“Kwa kipindi
chote ambacho nilikuwa nimebanwa na masuala ya ngumi, mradi wangu huu
uliyumba kwani kila niliyemwachia alikuwa na fikra za kuniibia, ilifikia
mahali nikakwama kwani nilikopa fedha benki kuongezea nguvu kwenye
biashara yangu ya makopo hivyo nilipaswa kulipa,” anasema Cheka.
Anavyookota chupa mtaani
“Watu
wanashangaa mtu kama mimi kuokota chupa, lakini ndiyo kazi inayoniweka
mjini, wiki iliyopita nilikuwa Msamvu (stendi kuu ya Morogoro) nakusanya
chupa kwa bahati nikakutana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alishangaa kuniona naokota Chupa.
“Hakuamini
kama mimi bingwa wa dunia na bondia namba moja Tanzania ndiyo naokota
chupa mtaani, lakini ukweli nisipofanya kazi hii na nikabaki kutegemea
ngumi, maisha yatakuwa magumu kwangu,” anasema Cheka.
Anasema
haoni aibu kufanya kazi hiyo kwani ni kazi iliyompa mafanikio na kujenga
nyumba mbili, moja ikiwa Kilimahewa ambako anaishi hivi sasa na
nyingine Kihonda alikowapangisha watu wengine.
“Muda wangu
mwingi nimeelekeza kwenye chupa, mazoezi sasa sifanyi kwani nina muda
sijafanya mazoezi ya ngumi, nasimamia mwenyewe biashara yangu ya chupa
ambayo mbali na kuokota mwenyewe pia kuna watu ambao wanaokota na
kuniuzia.
“Chupa za
maji nanunua kilo moja Sh250 na mimi nauza 700 baada ya kusaga, kwa
mwezi nina uhakika wa kuuza kilo 4,500 mpaka 6,000 na plastiki ngumu
nanunua Sh350 na mimi nauza Sh 2,000 baada ya kusaga hivyo kwa mwezi
nauza zaidi ya kilo 3,000, pia naokota chupa za konyagi na chibuku
ambazo naziosha na kuwauzia watu wa kampuni hizo,” anasema Cheka.
Ameamua kuingia mtaani kutembeza CD
“Sijapata
mafanikio yoyote kwenye ngumi hadi sasa hivyo nimeona nijaribu kuuza CD
za mapambano yangu labda nitafanikiwa,” anasema Cheka.
Anasema kazi
hiyo anaifanya kwa kutembeza CD zake mkononi na kuwapelekea watu kwenye
maeneo tofauti mjini Morogoro na amekwishauza CD 200 hadi sasa.
“Nilitoa CD
200 ambazo niliziuza kwa kutembeza mwenyewe mkononi zikaisha na sasa
nimetoa nyingine 200, najitangazia biashara mwenyewe kwani napeleka
kwenye mkusanyiko wa watu, vituo vya daladala, Stendi ya Msamvu na
maeneo ambayo najua nikienda sikosi wateja, CD moja nauza Sh 3000,”
anasema Cheka.
Fedha nyingi aliyowahi kupata katika ngumi
“Fedha
nyingi niliyopata ni Sh10 milioni ambayo nilicheza pambano Russia mwezi
Desemba 2012 na kupigwa kwa Knock Out (KO) raundi ya nne, pambano lile
nilicheza bila kujiandaa na nilipata fedha hiyo kwa kuwa sikuitumia
kwenye maandalizi,” anasema Cheka.
Anasema
mapambano mengi anayocheza nchini amekuwa akiambulia Sh3 milioni mpaka
Sh4 milioni baada ya kutoa fedha za maandalizi, kumlipa kocha na kununua
vifaa.
“Pambano
nililocheza na Mmarekani la ubingwa wa dunia nilipewa Sh4 milioni za
maandalizi, nikaweka kambi Nairobi kila kitu nalipa mwenyewe mpaka
kumlipa kocha, hadi narudi sina fedha baada ya pambano nikapewa Sh3
milioni, nilikuwa na madeni nikalipa na kubaki sina kitu.
“Hata wakati
nafanyiwa sherehe ya kupongezwa Morogoro, sikuwa na hata shilingi, siku
nawekewa dau la Sh10 milioni nikacheze Russia, sikukataa japo nilijua
sina mazoezi, nilipigwa KO kihalali na kuvuliwa ubingwa wa dunia,”
anasema Cheka.
Mkakati wake wa kurudi shule
Cheka
alipewa ofa ya masomo kwenye Chuo cha St Joseph cha mjini Morogoro na
aliingia darasani siku moja kisha akatokomea hadi leo hajawahi kurudi.
“Mimi ni
baba wa familia ambayo inanitegemea, siyo kama sipendi kusoma, lakini
nikiwa shule majukumu ya familia nitayatekeleza vipi? Hivi sasa nimeamua
habari ya kusoma niiweke kando niboreshe biashara yangu, Mungu
akiniweka hai, nitasoma miaka ijayo,” anasema Cheka.
Kwa nini anaitwa Kazimoyo?
Akiwa Morogoro, Cheka anajulikana pia kwa jina la Kazimoyo.
“Hili jina
nimepewa na marafiki zangu ambao wananiita Kazimoyo kutokana na kazi
ninazozifanya, ambazo wanasema nina moyo mgumu ndiyo sababu nazifanya,
hivyo kazi ninazofanya sasa na nilizowahi kufanya nimefanya kwa moyo
tu,” anasema Cheka.
Historia fupi ya maisha yake
Cheka
alizaliwa miaka 32 iliyopita jijini Dar es Salaam, akiwa mtoto wa kwanza
kwa baba yake, Boniface Cheka na alisoma Shule ya Msingi Kinondoni
Hananasifu.
Alianza kucheza ngumi akiwa darasa la tatu na wakati huo baba yake alipenda kumfundisha ngumi.
“Nilipohitimu
shule ya msingi, nilipata kazi kwenye gari la taka la Manispaa ya
Kinondoni, nilifanya kazi hiyo pia nikijifua ngumi kwenye Ukumbi wa
Arnautoglu, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Baada ya
kuona maisha magumu Dar es Salaam, Nilikwenda Morogoro, sikuwa na mahali
pa kufikia hivyo nikaomba kazi ya kufagia Stendi ya Msamvu na usiku
hapo ndipo nikawa nalala,” anasema Cheka.
Anasema
alilazimika kutandika maboksi na kulala kituoni hapo usiku ulipoingia na
asubuhi anaamkia kwenye kibarua cha kufagia kituo hicho.
“Nilipata
fedha kidogo na kupanga chumba, nakumbuka kitanda changu nilinunua kwa
fedha niliyopata kwenye kazi ya kuzibua choo, sikuwa na ujuzi huo,
lakini rafiki zangu waliponiambia kuna kazi hiyo nilienda kufanya na
kulipwa Sh50,000 ambayo ilikuwa fedha nyingi kuwahi kulipwa,” anasema
Cheka.
Anasema
baada ya muda ndipo aliingia mtaani kuokota chupa, kazi iliyompa
mafanikio na kujenga nyumba, na kutumia fedha aliyopata kujitangaza
kwenye ngumi.
CREDIT: MWANANCHI
No comments :
Post a Comment